MWENGE WA UHURU MKOANI ARUSHA 2019.
Mkoa wa Arusha unatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru tarehe 6 Juni, 2019 katika Wilaya ya Ngorongoro kata ya Ololosokwani ukit5okea Mkoa wa Mara.
Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Wilaya 6 za Mkoa wa Arusha na Halmashauri zake 7, ukianzia Wilaya ya Ngorongoro, Longido, Arusha,Meru, Jiji la Arusha,Monduli na kumalizia wilaya ya Karatu.
Mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani Arusha utafanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kuzindua, kufungua na kukagua miradi 57 ya maendeleo ya wananchi yenye thamani ya Tshs. Bilioni Mia Tano Sabini na Nane Milioni Mia Tatu Sitini na Laki Tisa na Arobaini Tano Elfu, na Mia Moja Sabini na Mbili na Senti Hamsini (578,360,945,172.50) kwa mchanganuo ufuatao:-
Miradi 15 itawekwa jiwe la msingi, miradi 4 itafunguliwa, miradi 12 itazinduliwa na miradi 26 itatembelewa na kukaguliwa kuona maendeleo yake. Miradi hii ni ya maji, afya, ujenzi wa barabara, elimu, utawala, kilimo, uvuvi, ufugaji, uhifadhi wa mazingira na miradi mingineyo.
Aidha mbio hizi zitakagua na kupokea taarifa ya ukamilishaji na uendelevu wa miradi iliyopitiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 pamoja na uwezeshaji wa vijana na watu wenye ulemavu kiuchumi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri zetu kwa mgawanyo wa 4% kwa vijana na 2% kwa watu wenye ulemavu.
Ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila Mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
Aidha kaulimbiu hii inaambatana na ujumbe wa kudumu kuhusu mapambano dhidi ya:-
VVU/UKIMWI, chini ya kauli Mbiu isemayo “Pima, Jitambue, Ishi”
Malaria, chini ya kauli Mbiu isemayo “Nipo tayari kutokomeza Malaria, wewe Je?”
Dawa za kulevya, chini ya kaulimbiu isemayo “Tujenge Maisha Yetu, Jamii Yetu na Utu Wetu bila Dawa za Kulevya”
Rushwa, chini ya kaulimbiu isemayo “Kataa Rushwa, Jenga Tanzania”
Mwenge Uhuru utakabidhiwa kwa Mkoa wa Manyara mnamo tarehe 13 Juni, 2019.
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Habari na Uhusiano,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.