Kila mwananchi anaemiliki ardhi anatakiwa kuhakikisha amepata hati miliki ya ardhi yake ndani ya siku 90 baada ya zoezi la upimaji kukamilika kipindi cha nyuma katika eneo lake na siku 7 kwa aliyepimiwa hivi karibuni.
Yamesemwa hayo na Waziri wa ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvu alipokuwa akifungua ofisi mpya za ardhi kwa Mkoa wa Arusha na kugawa hati miliki kwa wananchi wapatao 200 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha mapema leo hii.
Amesema kila mwananchi anaemiliki ardhi ana haki ya kupatiwa hati miliki ili aweze kuwa mmiliki halali wa eneo husika.
Lukuvu amesema pia hata waliojenga mijini nao wanahaki ya kupatiwa hati miliki baada ya kupimiwa na kulasimishwa kwa maeneo yao.
Kutokana na kufunguliwa kwa ofisi za ardhi za Mkoa Lukuvu amesema, huduma zote za ardhi zitakuwa zinapatikana hapo na kuwataka wananchi wote kuzitumia kwa changamoto zao zote za maswala ya ardhi.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Kimanta amesema atahakikisha migogoro yote ya ardhi anaitatua na itabaki kuwa historia tu kwa mkoa huu.
Amesema serikali ya Mkoa itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa ofisi hiyo ya ardhi hasa kwa kuhakikisha ndani ya siku 7 inaipatia ofisi kubwa ya kukidhi mahitaji yao.
Pia, ametoa fursa ya kuongeza siku za kusikiliza malalamiko kwa wananchi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutoka siku 2 za awali hadi siku 5 za kazi katika wiki nzima.
Aidha, amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanaitumia hiyo ofisi vizuri katika kutatua matatizo yote yanayowahusu kuhusu maswala ya ardhi.
Katibu Mkuu Wizara ya ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Doroth Mwanyika amesema,lengo kubwa la kuanzisha ofisi hizi za ardhi katika mikoa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa lengo la kusogeza huduma karibu kwa wananchi.
Pia,kuhakikisha kero zote za wananchi zinatatuliwa kwa wakati na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mpango wa kufungua ofisi za ardhi za Mikoa unatekelezwa katika Mikoa yote ya Tanzania bara kwa nia ya kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kufuata mchakato hadi Wizarani.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.