Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amelitaka jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kujikita katika kufanya tafiti zitakazowesha kupata Suluhu za kudumu za kupunguza ajali za barabarani.
Maagizo hayo ameyatoa alipokuwa akifungua maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani Kitaifa,Jijini Arusha.
Amesema zikifanyika tafiti nyingi za kitaalami zitasaidia kupata suluhu ya kudumu ya kupunguza ajali za barabarani au kuzuia kabisa ili kuokoa vijana wengi wanaopoteza maisha kwa wingi.
Ajali nyingi za barabarani zaidi ya asilimia 90 zinasababishwa na makosa ya kibinadamu huku asilimia 3.2 za ajali zinatokana na ubovu wa magari na asilimia 1.3 ni ubovu wa Barabara.
Kutokana ma sababu hizo jumla ya watu waliopoteza maisha ndani ya miaka mitano ni 2220 kwa ajali za bodaboda, majerui 4402 na kwa mwaka vijana takribani 445 walikuwa wamepoteza maisha.
Pia, ajali zingine zilizotokana na basi zilikuwa 148 na daladala 142, kutokana na takwimu hizo bado bodaboda wanaongoza kwa vifo nchini, hivyo elimu iendelee kutolewa zaidi kwao.
Vile vile amesisitiza katika ukaguzi wa magari kwa njia za kisasa hasa katika zoezi la utoaji stika za nenda kwa usalama katika magari ili kurahisha ukaguzi kwa magari mengi na kulipatia fedha jeshi la polisi zitakazo saidia kuendesha shughuli zao mbalimbali.
Nae, Katibu mtendaji wa balaza la Taifa la usalama barabarani kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi SACP Wilbrod Mutafungwa amesema, hadi sasa ajali za barabarani zinapungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Kwa mwaka 2020 jumla ya ajali za barabarani 1383 zilitokea na 2021ajali zilikuwa1187 ambazo ni punguzo la ajali 201 sawa na asilimia 14.5, huku vifo vikiwa 949 mwaka 2020 na 2021 vilikuwa 900 sawa na punguzo la vifo 49 sawa na asilimia 5.2.
Pia, katika mwaka huo majerui walikuwa 1672 kwa mwaka 2020 na 2021 walikuwa 1405 kwa punguzo la majerui 267 sawa na asilimia 16.
Ameainisha sababu kubwa za ajali za barabarani ni ubovu wa Barabara, kutovaa kofia ngumu kwa madereva, kutofuata Sheria za barabarani na nyingine nyingi.
Aidha, amewaomba wadau wa usalama barabarani kuendelea kuunga mkono juhudi za kuzuia ajali za barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amemshukuru Rais Samia Suluhu kwa kutoa fedha takribani Bilioni 20.6 kwa Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Arusha na bilioni 19 kwa Wakala wa barabara Vijijini na mjini (TARURA) kwa Mkoa wa Arusha ili kuboresha Barabara na kulinda usalama wa watu.
Maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani yamezinduliwa rasmi leo Novemba 23,2021 na yanatarajiwa kufungwa Novemba 28, 2021 ambapo mara ya mwisho yaliadhimishwa 2017 Mkoani Kilimanjaro na kauli mbiu ya mwaka huu ni" Jali usalama wako na wengine barabarani".
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.