Walipakodi wa Mkoa wa Arusha watakiwa kulipa kodi kwa wakati na kwa hiari ili kupeleka mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.
Yamesemwa hayo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika ufunguzi wa warsha ya walipakodi wakubwa wa mkoa wa Arusha.
Amesema ulipaji kodi kwa wakati na kwa hiari unaisadia serikali katika kutatua matatizo mbalimbali ya watanzania wa kawaida na wa hali ya chini ya maisha ili waweze kupata matumaini mapya katika maisha yao.
Kwitega amesema, ulipaji wa kodi unasaidia kubadili mfumo wa uchumi kuwa wa kipato cha kati kwa kukuza sekta ya viwanda ili kuongeza ajira hususani kwa vijana wetu.
Pia, kodi husaidia kuboresha huduma muhimu za jamii kama Barabara,Maji, Safi,Umeme wa uhakika na huduma za afya na pembejeo bora kwa wakulima.
Ametoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanyakazi kwa kuzingatia sheria za kodi,weledi, uwajibikaji na uadilifu wa hali ya juu na wachukue hatua stahiki kwa wale wote wanaokwepa kulipa kodi lakini bila kuonea mtu.
Akitoa taarifa fupi ya maboresho ya mifumo ya ulipaji kodi Mkurugenzi wa mamlaka ya mapato Tanzania tawi la Arusha bwana Faustine Mdesa amesema TRA imeboresha mifumo ya ulipaji kama vile kodi ya zuio kwa njia ya mtandao ambayo imerahisha malipo na upatikanaji wa vyeti vya malipo.
Bwana Mdesa amesema pia, kuna maboresho ya sheria ya ushuru wa bidhaa ili kuongeza tija katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na rasilimali za Taifa.
Amesisitiza zaidi faida kubwa ya maboresho hayo kumeongeza ufanisi wa utunzaji wa kumbukumbu za kodi ya zuio kwani sasa malipo yote ya kodi ya zuio huingia moja kwa moja kwenye akaunti ya mlipakodi husika.
Na wahusika wote hupata vyeti vya zuio pindi tu malipo yanapofanyika benki.
Mamlaka ya Mapato Tanzania wamekutana na walipa kodi wakubwa wa Jijini Arusha kwa lengo la kuwapa elimu zaidi juu ya maboresho ya mifumo ya malipo ya kodi iliyofanywa na mamlaka hiyo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.