Na Elinipa Lupembe.
Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Rasilimali watu, David Lyamongi, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K. Mongella kwenye Kongamano la 14 la mwaka la Wataalam wa Ununuzi na Ugavi nchini, kongamano lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha ( AICC), leo tarehe 12 Desemba, 2023.
Akitoa salama za mkoa wa Arusha, Lyamonge amesema kuwa Wataalam wa Manunuzi na Ugavi ni kiungo muhimu kwa taasisi zote za Serikali, hivyo wanatakiwa kuzingatia kanuni, sheria na taraibu za manunuzi na kuhakikisha kazi zote zinafanyika kidigitali kupitia mfumo wa NEST kama yalivyo maelekezo na matakwa ya Serikali.
"Wataalam wa manunuzi wawe chanchu kwa watumishi wengine katika manunuzi yanayozingatia sheria hasa kuwaelekeza matumizi sahihi ya mfumo wa Nest na kuachana na manunuzi ya nje ya mfumo ya kianalojia, ambayo ni kinyume na taratibu za Serikali" Amesema Lyamongi
Ameongeza kuwa kama yaluvgo malengo ya Kongamano hilo ni kubadilishana uzoefu kuhusu mabadiliko ya Kidigitali, katika kuboresha Usimamizi wa Mnyororo wa Ununuzi Ugavi kwa Maendeleo Endelevu, wahakikishe wanatoka na uelewa wa pamoja, utakaokwenda kuzisaidia Taasisi zao na Serikali kwa ujumla wake.
Aidha, ametumia fursa hiyo, kuwashukuru Bodi ya Wataalam hao, kuichagua Arusha kufanya mkutano huo muhimu kwa Serikali na kuwakaribisha mkoani Arusha na kuwaahidi ushirikiano huku wakiendelea kufurahia mandhari nzuri ikiambatana na hali ya hewa inayovutia ya mkoa wa Arusha pamoja na kuwahakikishia hali ya amani, utulivu na usalama wao kipindi chote watakapokuwa Arusha.
Awali, Kongamano hilo la siku tatu, limefunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, lenye lengo la kiwakutanisha pamoja watalaam wa fani hiyo ili kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili mada kuhusu mabadiliko ya Kidigitali, katika kuboresha Usimamizi wa Mnyororo wa Ununuzi Ugavi kwa Maendeleo Endelevu.
Kauli Mbiu ya Kongamano la 14 mwaka 2023 ni "Mabadiliko ya kidigitali katika kuboresha usimamizi wa mnyororo wa manunuzi na ugavi kwa maendeleo Endelevu"
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.