Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi wa Halmshauri nchini wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ili kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 9 Mei, 2024 wakati akifungua warsha ya Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za mikoa tisa ya Tanzania Bara kuhusu Usimamizi na Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyofanyika Jijini Dodoma.
“Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na Wakurugenzi dumisheni amani na mshikamano katika maeneo yenu ya kazi na kati yenu na wananchi ili kujenga taswira nzuri”amesema na kuongeza kuwa inasikitisha kuona viongozi wanaofanya kazi pamoja hawaelewani na hivyo kusabisha migogoro mahali pa kazi na pengine kusababisha hasara kwa Serikali.
Amesisitiza umuhimu wa viongozi kutekeleza majukumu yao na kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa, kushirikiana na Taaisi za Haki Jinai na kujipanga kutekeleza Mkakati wa Kubaini Uhalifu kabla hajatendeka badala ya kusubiri kukabiliana nao.
“Wekeni mkakati thabiti wa kuzuia migogoro ya ardhi na endeleeni kuweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyiakazi kwa kuzingatia sheria, Tatueni kero za wananchi kwa haki bila kumuonea mtu.” Amesisitiza Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa mada mbalimbali zitawasilishwa na wabobezi kutoka sekta tofauti, hivyo walengwa wajipange kupata maarifa na kuzingatia yote watakayoelekezwa katika warsha hiyo kwa ajili ya kuboresha utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Zainab Katimba amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume ya Haki Jinai na kuwa Ofisi yake ipo tayari kuhakikisha azma ya Rais Samia inafanikiwa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.