Elinipa Lupembe.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI anayesimamia Afya, Dkt. Wilson Charles Mahera, akizungumza kwenye mkutano wa hafla fupi ya Ugawaji wa Magari ya Afya kwa mikoa ya Arusha na Manyara, kwenye ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, tarehe 13 Desemba, 2023, amesema kuwa, Serikali imeendelea kuboresha utoaji na upatikananji wa huduma za afya nchini kwa kuboresha miundombinu katika sekta hiyo.
Dkt. Mahera, ameweka wazi kuwa, Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha jamii inapata huduma za afya kuanzia ngazi ya kijiji, imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba za watumishi wa afya, dawa, vifaa na vifaa tiba.
Hata hivyo, serikali katika kutekeleza hayo yote, imeenda mbali zaidi na kutoa magari 316 ya idara za Afya mikoa yote Tanzania, huku magari 256 yakielekezwa kwenye ufuatiliaji wa shughuli za afya kwenye mikoa na halmashauri.
Aidha, amewataka watumishi wa afya, kutumia magari hayo katika shughuli zilizoelekezwa na Serikali na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na stahiki, ikiwa ni pamoja na kupambana na vifo vya watoto na wamama wajawazito wakati wa kujifungua.
"Waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, tumieni magari haya kufanya ufuatiliaji, tokeni ofisini, nendeni kwenye vituo vya afya mkaone namna wagonjwa wanavyohudumiwa, hakikisheni wagonjwa wanapata huduma kwa wakati, isitokee mgonjwa anapoteza maisha kwa kucheleweshwa kupata huduma, serikali haitamvumilia mtumishi wa aina hiyo" Amesema Dkt. Mahera.
Ameongeza kuwa, kwa sasa vifo vya mama na mtoto vimepungua nchini, kutoa vifo 555 mpaka kufikia vifo 104 kwa kizazi hai kimoja, hii ni kutokana na taarifa aliyoipokea Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwezi Oktaba 2023, taarifan inayothibitisha namna Serikali ya awamu ya sita inavyofanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Awali, akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Mahera amesema kuwa, jumla ya magari 13 yatakabidhiwa kwa viongozi wa mikoa ya Arusha na Manyara, ambapo magari 5 kwa mkoa wa Arusha na magari 8 kwa mkoa wa Manyara, yote yakielekezwa kufanya shughuli za ufuatiaji shirikishi wa huduma za afya.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.