Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na waumini mara baada ya kushiriki Ibada ya Mwaka Mpya katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma. Amesema ni muhimu watanzania kuendelea kukemea na kupinga utengano, udini ukabila pamoja na siasa za chuki.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi watanzania kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ili kuinua maisha ya familia, jamii na taifa kwa ujumla. Pia amewaasa watanzania kulipa kodi halali ili taifa liweze kupata maendeleo ya haraka.
Makamu wa Rais amewataka watumishi wa umma na viongozi wa umma kutimiza wajibu wao ipasavyo wa kuwahudumia wananchi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kutenda haki wakati wote wanapotoa huduma. Amewasihi kufanya kazi kwa hofu ya Mungu na kuachana na tabia za kuwapa kesi wananchi wasiohusika na kesi hizo. Pia amesema ni vema viongozi wa umma wanapotunga sera na sheria kuhakikisha zinakuwa na manufaa kwa wananchi wengi.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuwaasa wananchi kuachana na tabia za uharibifu wa mazingira ikiwemo utupaji taka ovyo. Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na madhari nzuri inayovutia hivyo inapaswa kutunzwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Makamu wa Rais amesema kwa mwaka 2023 Serikali ya Sita ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile elimu, afya, miundombinu na maji. Ameongeza kwamba kwa mwaka 2024 serikali itaendelea kuimarisha demokrasia, utawala wa sheria, haki, amani na umoja.
Vilevile amewasihi wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule kwa mwaka huu 2024 wanaanza masomo yao na wakati wote kufuatilia maendeleo ya watoto hao shuleni
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.