Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Dkt.Athumani Kihamia amezisisitiza Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha ujenzi wa Madarasa na utengenezaji wa Viti, Meza na madawati unakamilika ifikapo Disemba 15,2021.
Maagizo hayo ameyatoa alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa madarasa katika Halmashauri ya Arusha yanayojegwa kwa fedha za tozo za miamala na fedha za mapambano dhidi ya UVIKO 19.
"Itakuwa haina maana kama mkimaliza madarasa kwa wakati bila Viti na Meza, maana wanafunzi hawataweza kuyatumia na maana halisi ya darasa ni liwe na Viti na Meza", alisisitiza.
Serikali imetoa fedha nyingi kwa lengo la kuondoa changamoto ya wanafunzi wanaotakiwa kujiunga kidato cha kwanza kuchelewa kuanza masomo.
Jukumu letu ni kuhakikisha tunamaliza haya madarasa kwa wakati tuliowekewa kwani Rais Samia Suluhu yeye ameshamaliza kazi yake ya kutoa fedha baada ya kuona kuna changamoto ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kuchelewa kuanza masomo.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala amekagua ujenzi wa Madarasa 11 shule ya Sekondari Ilkidinga yaliyogharimu Milioni 220, shule ya Sekondari Kiranyi madarasa 13 yenye thamani ya Milioni 260, shule ya Sekondari Mringa madarasa 10 Milioni 200.
Shule ya Sekondari Lengijave darasa moja la Milioni 20, shule ya Sekondari Oldonyosambu madarasa 2 ya thamani ya Milioni 40, shule ya Sekondari Oldonyowas darasa moja la Milioni 20, shule ya Sekondari Mateves madarasa 3 Milioni 60 na shule ya Sekondari Einot madarasa 4 yenye thamani ya Milioni 120.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha bwana Selemani Msumi amewataka walimu wakuu wa shule za Sekondari za Halmashauri hiyo kuongeza muda wa kusimamia ujenzi wa Madarasa hayo hata nyakati za usiku wafunge taa ili kasi ya ujenzi iongezeka.
Aidha, amewapongeza walimu wa shule hizo kwa ushirikiano waliouwonesha unaopelekea ujenzi wa Madarasa kwenda kwa kasi, hivyo ameomba waendelee na ushirikiano huo ili kufanikisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.
Halmashauri ya Arusha ilipatiwa fedha kiasi cha Bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa 100 ambapo 96 ni madarasa ya Sekondari na manne ni madarasa ya shule shikizi 2, hata hiyo kwa Mkoa mzima wa Arusha fedha kiasi cha Bilioni 8.5 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa ya shule za Sekondari na shikizi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.