Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amezitaka Mamlaka zote za Urekebu na udhibiti zilizopo nchini Tanzania kuhakikisha wanawasaidia na kuwalea wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao nchini ili kuweza kufanya biashara zao kwa uhuru na kwa faida bila ya usumbufu wa kimfumo.
Prof. Kitila ametoa kauli hiyo mapema leo Julai 04, 2024 kwenye ukumbi wa Jengo la Ngorongoro Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya kituo cha uwekezaji TIC kanda ya Kaskazini na uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya uhamasishaji wa uwekezaji wa ndani.
Katika hatua nyingine Profesa Kitila Mkumbo amesema mamlaka zote hizo zitaunganishwa pamoja na kufanya kazi kidigitali kwenye kituo hicho cha pamoja ili kumfanya mfanyabiashara na mwekezaji kulipa tozo mara moja na kupata leseni moja badala ya kuwa na utitiri wa leseni kama inavyofanyika sasa.
Kulingana na Waziri Kitila Mkumbo, TIC imeamua kuweka ofisi zake za kanda mkoani Arusha zikitokea mkoani Kilimanjaro, kutokana na umuhimu wa mkoa wa Arusha katika uchumi wa nchi pamoja na fursa mbalimbali za kiuwekezaji zinazopatikana katika mkoa huu ulio kitovu cha utalii kanda ya Kaskazini.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.