Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema kuwa, Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yaliyopngwa kuanza mkoani humo Juni 7 mwaka huu, yanatarajiwa kuchochea na kusisimua kwa kiasi kikubwa Utalii huku akiwataka wananchi na Wadau wa Utalii kuchangamkia fursa ya uwepo wa maonesho hayo.
Mhe. Makonda amesema hayo, alipotembelea na kukagua maandalizi ya maonesho hayo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Magereza Arusha, mapema leo Juni 5, yanayotarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Maliasili na utalii Mhe. Angellah Kairuki.
Aidha, maonesho hayo yanatarajiwa kushirikisha Makampuni ya Kimataifa zaidi ya 700 kutoka takribani Mataifa 50 na yakitarajia kushirikisha Makampuni wenyeji zaidi ya 500 yatakayoonesha bidhaa na kazi mbalimbali kwenye maonesho hayo.
"Niwasihi wadau wa utalii kushiriki kikamilifu kwenye maonesho haya ili kutangaza huduma zenu pamoja na kubadilishana uzoefu na makampuni mengine ya ndani na nje ili kusaidia kukuza utalii Arusha na Tanzania kwa ujumla wake". Amesisitiza Mhe. Makonda
Hata hivyo, ametumia fursa hiyo, kuwakaribisha wananchi na raia wote wa kigeni kwenye maonesho hayo, akiwahakikishia suala la ulinzi na usalama muda wote wa maonesho hayo yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kili Fair, Dominic Shoo, amemuambia Mhe.Makonda kuwa, tayari maandalizi yamekamilika 95% akisisitiza kuwa maonesho ya mwaka huu yameboreshwa zaidi, ikiwemo kuongeza saa za maonesho hayo pamoja na kutenga maeneo maalum kwaajili ya michezo ya watoto.
Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 yanafanyika kwa awamu ya tisa Jijini Arusha likiwa ni jukwaa maalum la kuyaweka pamoja makampuni ya ndani na nje ya nchi yanayohusika na sekta ya Utalii ili kuwakutanisha pamoja na kubadilishana bidhaa, huduma na uzoefu unaotokana na sekta ya Utalii duniani.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.