Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mha. Cyprian Luhemeja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa mapambano ya mabadiliko ya Tabianchi.
Ameyasema hayo, wakati wa ziara ya kikazi ya Wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa 35 wa Kamati ya Kudumu ya Fedha ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), walipokiwa wakiangalia Mradi wa kuboresha Usimamizi wa Malisho katika Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Randilen, Monduli mkoani Arusha.
Ameongeza kuwa mabadiliko ya Tabianchi ni vita ambayo kila mtu anapaswa kupigana ndio maana kwa mara ya kwanza Tanzania inaandaa Mkutano Mkubwa wa UNFCCC utakaoanza kesho Septemba 2,2024 mkoani Arusha wenye lengo la kujadili hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
”Ajenda kubwa ya mwaka huu kwenye mkutano huo ni mabadiliko ya Tabianchi na jinsia na kimsingi wanaangalia namna ya kuokoa mama na mtoto kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi wao ndio wanaoathirika zaidi sababu maji yakipotea wao ndio wanapata taabu na chakula nyumbani mama ndiye muandaaji.
"Dunia imekutana Arusha, huu ni mkutano wa siku sita na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, hivyo ni bahati kubwa kwa nchi kuandaa mkutano huu,” amesema Mhe. Luhemeja.
Naye Mshauri wa Rais,kwenye masuala ya mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi amesema jambo la kwanza ni kumshukuru Mhe. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mkutano huu kufanyika Tanzania.
"Mataifa zaidi ya 50 yapo Tanzania na kikubwa wamefurahi kuona juhudi ya serikali inavyofanya katika kukabilina na mabadiliko ya tabianchi na imekuwa faraja kwa Watanzania kuona namna Randilen ilivyojitahidi katika kulinda na kuhifadhi mazingira,” amesema Dkt. Muyungi.
Amesisitiza kuwa pamoja na changamoto lakini Taifa limekuwa likiweka jitihada mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa kina mama namna ambavyo wamekuwa mstari wa mbele katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.
Naye Mshauri Mkuu wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Umoja wa Ulaya Bi. Apollonia Miola kutoka Italia amesema amefurahishwa kuona serikali ya Tanzania inavyoshirikisha jamii katika kulinda na kutunza Mazingira kupitia miradi mbalimbali.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.