Waziri mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa jiji la Arusha Dkt.John M.Pima kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia,Mheshimiwa Waziri Mkuu amewasimamisha kazi watumishi wengine watano wa Halmashauri hiyo akiwemo muweka hazina Bi.Mariam Mshana, wachumi watatu Innocent Maduhu, Alex Tlehama, Nuru Ginana na Joel Mtango Afisa manunuzi Halmashauri ya Longido kupisha uchunguzi huo.
Mhe. Majaliwa amemwagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali CAG pamoja na kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha kufanya uchunguzi wa kina wa matumizi hayo ya fedha na atakae bainika hajahusika atarudishwa kazini na atakaebainika amehusika hatua zaidi zitachukuliwa.
Aidha, amewasihi watumishi wote wa umma kufanya kazi kwa ushirikiano na kuboresha mahusiano baina yao ili kuongeza ufanisi zaidi kazini.
Amewataka watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi yenye staha na unyenyekevu kwani hayo ndio maelekezo ya Serikali.
Amesisitiza pia,kuwe na uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri ili kujenga uwelewa wa pamoja kwa madiwani na watendaji.
Mhe. Majaliwa amefanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Arusha na ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la ufundi katika chuo cha ufundi Arusha na amekagua masoko manne ya Machinga.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.