Na Elifuraha Laizer
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (MB), amesema, matumizi ya mfumo wa PIPIMS, PEPMIS na HR Assesment katika Utumishi wa Umma nchini, inakuja kufanya tathmini kwa watumishi wa Umma pamoja na kuwabana Watumishi wasiotekeleza majukumu yao na kufikia malengo yaliyowekwa.
Mhe.Kikwete amesema hayo, wakati akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kwenye kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha , 15 Desemba 2023.
Ameeleza kuwa, Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa kuhimiza uwajibikaji na kuhakikisha, Taifa linakuwa na utumishi wa Umma unaopimika kwa kumpima Mtumishi mmoja mmoja pamoja na Taasisi kwa ujumla.
"Mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa OPRAS, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, inayowezesha viongozi na watumishi wa Umma kuendelea kutekeleza majukumu yao, kwa ufanisi wakati na mahali popote, na zaidi kuwabana watumishi wanaopenda kukaa ofisini pasipo kufanya kazi" Amebainisha Naibu Waziri huyo
Aidha, Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala, kuacha kukaa ofisini badala yake, watembelee maeneo yote ya kazi, na kusikiliza changamoto zinaziwakabili watumishi walio chini yao na kuweza kuzitatua kwa wakati.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.John V.K Mongela, amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufuatilia utoaji wa mafunzo unaoendelea katika mkoa huo, na kusisitiza kuwa, kutokana na kukua kwa teknolojia, zama hizi hazihitaji watu wenye misuli badala yake wenye kuwajibika katika kazi.
Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, ambapo Maafisa Tawala, Utumishi na Rasilimali Watu, watabadilika kuendana na teknolojia na kuachana na utaratibu wao wa utendaji kazi wa kizamani.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kuwanoa upya Maafisa Tawala, Utumishi na Rasilimali Watu, wa mikoa na Halmashauri kwani utendaji wapo ambao utendaji kazi wao, sio wa kuridhisha, kwa kuzingatia, wao ndo wenye jukumu la kuwasimamia watumishi wengine.
#ArushaFursaLukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.