Viongozi wa Kata wa halmashauri zote za mkoa wa Arusha watakiwa kutafuta suluhu ya tatizo la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akitoa maagizo hayo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Arusha,mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahongo katika kuhadhimisha siku ya kilele cha wiki ya elimu Mkoani Arusha.
Amesema changamoto kubwa iliyopo katika sekta ya elimu Mkoani Arusha ni mimba kwa wanafunzi hasa wa Sekondari,ambapo kwa mwaka 2017 wanafunzi 237 waligundulika kuwa na ujauzito ikiwa wanafunzi 50 ni wa shule za Msingi na 187 ni wa Sekondari.
Aidha,kuanzia Januari hadi Aprili 2018 jumla ya wanafunzi 97 waligundulika kuwa na ujauzito ambapo wanafunzi 17 niwa shule za Msingi na 80 wa Sekondari.
“Bado tatizo la ujauzito kwa wanafunzi wa kike ni changamoto kubwa hasa wa sekondari,wazazi bado mna jukumu kubwa hasa la kuhakikisha mnasimamia maadili ya watoto wenu na pia kuchangia fedha za chakula mashuleni ilikupunguza vishawishi kwa wanafunzi hawa”.
Katibu Tawala msaidizi upande wa elimu bwana Gift Kyando,amesema changamoto nyingine iliyopo katika sekta ya elimu Mkoani Arusha ni baadhi ya watoto kutojua kusoma,kuhesabu na kuandika (KKK), kwa sababu watoto hao hawapatiwi elimu ya awali kwanza kabla ya kujiunga na elimu ya msingi.
Amesema mbali na changamoto hizo,elimu bure kwa Mkoa wa Arusha imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya uwandikishaji wa watoto darasa la kwanza.
Akisisitiza zaidi anasema mradi wa mpango wa kusaidia kusoma,kuandika na kuhesabu (LANES) umeweza kusaidia sekta ya elimu kwa kiasi kikubwa kwani mradi umeweza kuongeza Vitabu,Vifaa vya kufundishia na Vyombo vya usafiri,ambapo kila halmashauri itapatiwa kopyuta 3 za kusaidia utunzaji wa taarifa mbalimbali za wanafunzi.
Juhudi kubwa inaitajika katika kutoa kipaombele kwa watoto wenye ulemavu, kwani Mkoa unajumla ya watoto wenye ulemavu 614 ambao wanaitaji kuwa na madarasa maalumu lakini pia bado kuna baadhi ya wazazi wanawaficha watoto hao manyumbani.
Bwana John Isiriri ni mmoja wa wazazi waliohudhuria kilele cha wiki ya elimu,amesema ni kweli kuna tatizo kwa watoto wenye ulemavu kwa kutopewa kipaombale tokea katika ngazi ya familia zao na hivyo kupelekea wengi wao kukosa elimu.
Pia amesema tatizo la ujauzito kwa watoto wa kike bado ni changamoto kwa watoto wao hasa wa sekondari, lakini wazazi sasa wanatakiwa kusimamia maadili ya watoto wao na pia kuchangia chakula mashuleni ili kupunguza vishawishi kwa watoto wa kike.
Maadhimisho ya kilele cha wiki ya elimu hufanyika kila mwaka na mwaka huu 2018 kimkoa yamefanyika katika wilaya ya Karatu kwa lengo la kuhamasisha utoaji wa elimu bora kwa shule za mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.