@ortamisemi
Naibu Katibu Mkuu Ofisi Ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini, kuhakikisha wanasimamia thamani ya fedha katika Miradi mbalimbali ya Afya inayotekelezwa katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Grace amesema wakati akifungua mafunzo ya mpango wa uwekezaji wa huduma za Afya ya Mama na Mtoto (TMCHIP) yaliyofanyika mkoani Morogoro yakihusisha Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, Wahandisi majengo, Maafisa Ugavi, Maafisa Mipango, Wahasibu, PPRA,Waratibu wa Miradi, Makatibu wa Afya na Waganga wafawidhi kutoka katika mikoa 17 na Halmashauri 25 ambapo mradi huo umeanza kutekelezwa.
“Kila mtaalamu aliyehudhuria hapa akasimame kwenye nafasi yake, popote pale ambapo mradi utaharibika hakuta kuwa na visingizio hatua stahiki zitachukuliwa kwa sababu wote mpo hapa kama timu moja ya utekelezaji wa mradi huu, hivyo nasisitiza miradi hii ya ujenzi iendane na thamani ya fedha inayotolewa na iishe kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi” Dkt Grace.
Mpango huu wa uwekezaji kwenye huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto (TMCHIP) unagharimu zaidi ya dola za kimarekani Mil.275 Kwa ushirikiano kati ya Benki ya Dunia, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya Tanzania Bara na Wizara ya Afya Zanzibar.
Mradi huu umejikita katika ujenzi na ukarabati wa vituo vya Afya, ununuzi wa vifaa na vifaa tiba, ajira za watumishi, mafunzo ya watumishi, usimikaji wa mifumo ya TEHAMA na uimarishaji wa huduma za rufaa kwa lengo la kuboresha huduma za afya na hasa za Uzazi na Mtoto. Huu ni mwendelezo wa jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vile vya watoto wachanga.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.