Na Elinipa Lupembe.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (MB), amewasihi watanzania, kutoa muda kwa TANESCO, ili shirika liweze kufanya maboresho ya miundombinu ya umeme, na kumaliza changamoto za kukatika umeme, ambayo ni kero kubwa kwa watanzania kijamii na kiuchumi.
Mhe. Biteko ametoa rai hiyo, wakati akizungumza na hadhara ya wakazi wa Arusha, mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusafirisha Umeme cha Lemuguru Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, kituo kinachojengwa njia kuu ya umeme wenye Msongo wa Kilovoti 400, kutoka Singida mpaka Namanga kueleleka Kenya, (Kenya-Tanzania Power Interconnection Project -KTPIP).
Ameweka wazi kuwa, licha ya kuwa TANESCO inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu na upungufu wa miundombinu, wizi pamoja na wadaiwa sugu wanaozorotesha uendeshaji wa shirika, kwa sasa Serikali inazishughulikia changamoto hizo na kuahidi kuwa ni lazima zipatiwe ufumbuzi wa haraka ili wananchi wapate umeme wa uhakika kwa muda wote.
"Kuna upungufu wa vituo vya kupooza umeme 95 nchi nzima, lakini TANESCO Arusha inao wadaiwa sugu wanaodaiwa takribani shilingi Bilioni 7.7, na wadaiwa wakubwa zaidi ni wafanyabiashara wakubwa na Taasisi, ninawapa rungu TANESCO, kufuatilia ulipwaji wa madeni hayo ya halali na kwa wale watakaokaidi, kukateni umeme mara moja" Amesisitiza Mhe. Biteko
"Wapo wanaodaiwa madeni makubwa na hawana mipango ya kulipa lakini wanataka huduma ya umeme, ninaagiza wadaiwa wote kulipa madeni hayo, tofauti ya hapo TANESCO kateni umeme bila kuangalia sura" Amesema
Hata hivyo, ameliagiza shirika la TANESCO, kuwa na mkakati thabiti wa kusikiliza kero za wananchi, ikiwemo uimarishaji wa vituo vya miito ya simu, pindi wananchi wanapohitaji kupata huduma na ufafanuzi kwa njia ya simu, wajibiwe, kwa kuwa kitendo cha kutokupata huduma hiyo wakati wanapokuwa na dharura, kinawaudhi watanzania, wanahitaji kusikilizwa na kutatuliwa dharura ya umeme, wacheni kuwawekea miito ya miziki ya kuhudumiwa.
Aidha amewaagiza watu wa kitenho cha dharura 'Emergency', kubadilika kwa kutatua kero za watanzania kwa wakati kero ambazo ziko ndani ya uwezo wa Shirika.
"Mkurugenzi wa TANESCO usicheke na watumishi wasiowajibika kuendana na kasi yetu, mtumishi yoyote anayekuvuta shati nyuma asivumiliwe, hatuwezi kuvumilia watumishi wazembe, wananchi wanahitaji umeme, TANESCO, boresheni huduma zenu, watu waone umuhimu wa nishati hii badala ya malalamiko" Amesema Naibu Waziri Mkuu
Amewathibitishia wana Arusha kwa, uwepo wa bwawa la mwalimu Nyerere, utachochea uwepo wa umeme wa uhakika, hivyo ni lazima vyanzo vya maji vikalindwa ikiwemo kutunza mazingira kwa kutokukata miti ovyo na kuwathibitishia ifikapo mwezi Machi mwaka 2024, suala la umeme litakuwa historia nchini kutokana na uwepo wa bwawa la Nyerere na kuagiza TANESCO katika suala la mazingira ni lazima washirikiane na NEMC ili kuhakikisha miundombinu ya TANESCO inalindwa.
Naye Mratibu wa Usimamizi wa mradi huo, Mhandisi Peter Kigadye amesema, mradi huo wa Kilovoti 400/220/33 kV wenye gharama ya shilingi bilioni 14.295, unaotarajia kukamilika February 28,2024 ambapo kwa sasa kazi za ujenzi zimekalika kwa asilimia 30 na kituo hicho cha kupooza umeme kitapeleka umeme katika wilaya za Monduli, Longido, Arumeru na Jiji la Arusha
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya kitanzania ya N/S Central Electical Tanzania Ltd na unafadhiliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.