Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega amewapongeza waoneshaji wote waliojitokeza mapema katika kuanza maandalizi ya sherehe za nanenane Kanda ya Kaskazini.
Ametoa pongezi hizo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwaja vya nanenane vilivyopo Themi Njiro Mkoani Arusha.
Amesema kwa niaba ya Makatibu Tawala wa Mikoa yote ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro na Manyara,wamefurahishwa na mwitikio mkubwa ulioneshwa na wafanyabiashara pamoja na wakulima katika kushiriki maandalizi ya sherehe hizo.
Kwitega amesema, mwaka huu maonesha hayo yatakuwa ya pekee sana kwani maandalizi yameanza mapema sana na hivyo kutoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara kujiandaa vya kutosha.
Maonesho hayo kwa mwaka huu 2020 yamebeba kauli mbiu isemayo “ Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi chagua viongozi bora 2020”.
Aidha, ametoa wito kwa wafanyabiashara wote,wakulima na wananchi kwa ujumla wa Mkoa wa Arusha kuendelea kufanya maandalizi ya sherehe hizo mapema huku wakichukua taadhari juu ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Corona).
Pia, Kwitega amesema bado nafasi zipo kwa wafanyabiashara na wakulima wanaopenda kushiriki maonesha ya nanenane 2020 na wanakaribishwa.
Maonesho ya nanenae kanda ya Kaskazini yanatarajiwa kuanzi Agost 1 hadi 8, 2020 na yatakuwa chini ya usimamizi wa serikali kwa awamu ya nne hadi sasa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.