Nchi za Afrika zimetakiwa kujenga mtaji wa Rasilimali watu kwa ajili ya karne ya 21, kwa kutoa elimu inayohusu mafunzo jumuishi ya kudumu katika maisha yanayoendana na changamoto za nchi zao, kuendana na mabadiliko ya kidijitali kisayansi na kiteknolojia.
Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango wakati akifungua Kongamano la Elimu kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Maadhimisho ya mwaka wa Elimu wa Umoja wa Afrika, kongamano linalofanyika mkoani Arusha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Ukumbi wa Simba Agosti 13, 2024.
Amesema kuwa nchi ya Tanzania imefanya mapitio katika mfumo wa elimu kwa kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu na kufanikiwa kugawanya elimu ya sekondari katika mikondo miwili, ikilenga elimu ya jumla na elimu ya ufundi stadi.
Aidha, ameweka wazi kuwa, mabadiliko hayo ya mfumo wa elimu yamelenga kuboresha ubora wa elimu katika mabadiliko ya kidijitali na mambo mapya ya kiteknolojia ndani ya mfumo wa elimu, ambapo wapo wanafunzi watahitimu na cheti cha shule ya sekondari na wengine cheti cha mafunzo ya ufundi stadi.
"Tunafanya hivi ili kuhakikisha kuwa mfumo wetu wa elimu unatoa fursa za kutosha kwa wale wanafunzi ambao uwezo wao uko zaidi kwenye ujuzi badala ya taaluma ya Fauci tulifanya hivyo kwa kutambua ukweli kwamba moja ya kikwazo cha kuvutia uwekezaji katika nchi yetu ni ukosefu wa ujuzi wa kutosha."
Hata hivyo amebainisha kuwa, maboresho hayo yatahusisha uwekezaji katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya kupata elimu inaoyendana na ongezeko la idadi ya walimu na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kidijitali.
Licha ya kuwa lengo ni kuboresha ubora lakini zaidi ni kuhakikisha kuwa elimu inampa mwananfunzi ujuzi na maarifa yanayoendana na ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya haraka ya kiteknolojia.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.