Wafanyakazi serikalini wametakiwa kuheshimiana bila kujali vyeo vyao walivyonavyo katika nafasi zao.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta, alipokuwa akizindua baraza jipya la wafanyakazi ngazi ya Mkoa,jijini Arusha.
“Nendeni mkahakikishe watumishi wa umma wanaheshimiana bila kuangalia vyeo vyao walivyonavyo,hii itasaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwenu”.
Kimanta amelitaka baraza hilo likawe shirikishi na kusimamia utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wa serikali na utoaji huduma bora kwa wananchi.
Nae, mwenyekiti wa Baraza hilo ambae pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega amesema, baraza hilo linakazi kubwa ya kuhakikisha linasimamia maelekezo yote yanayotolewa na serikali kwa watumishi wa umma ili yatekelezwe.
Aidha, amewataka wajumbe hao wa baraza ambao ni wawakilishi wa wafanyakazi wa serikali katika nafasi mbalimbali,kwenda kufanya kazi kwa bidii hasa kwa kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi.
Baraza jipya la wafanyakazi ngazi ya Mkoa limezinduliwa rasmi baada ya baraza lililopita kumaliza muda wake wa kuhudumu wa miaka 3.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.