Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo Gerson Msigwa amewataka wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani kuwa walinzi wa miundombinu ya miradi ya Maji katika Jiji hilo.
Ameyasema hayo alipokuwa akitembelea na kukagua mradi mkubwa wa Maji safi na usafi wa mazingira Jijini Arusha.
"Huu mradi ili uweze kudumu vizazi vingi unatakiwa kulindwa na wananchi wenyewe hasa miundombinu yake".
Msigwa amesema mradi huo utagharimu bilioni 520 na ni mradi wa pili kwa kupatiwa fedha nyingi Tanzania baada ya mradi mkubwa wa Maji uliopo Mkoani Mwanza.
Mradi huo wenye visima 56 ambavyo ni vya kwanza kwa urefu nchini Tanzania, utawanufaisha wananchi zaidi ya laki sita ndani ya Jiji la Arusha na maeneo ya jirani.
Aidha, Msigwa amewataka wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (AUWASA) kutoa huduma bora kwa wananchi huku wakilinda miundombinu ya miradi ya Maji kwani Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Maji ili huduma ya maji iwafikia wananchi kwa ukaribu.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira(AUWSA) Mhandisi Justine Rujomba amesema kupitia mradi huo wa bilioni 520 mamlaka imeweza kuongeza wateja wake wapya takribani 4500 wameshapatiwa huduma ya maji.
Pia, Mhandisi Rujomba amesema kupitia mradi Akimkosa, amesema wataweza kutoa huduma ya usafi wa mazingira kutoka asilimia 7.66 hadi asilimia 30 yenye idadi ya watu 201,811 kutoka watu 30,000.
Amesema mradi huo ulianza Novemba 2017 na unatarajiwa kukamilika Juni 2023 ukiwa umegharimu kiasi cha bilioni 520 fedha kutoka Serikali ya Tanzania na benki ya maendeleo Afrika (AfDB).
Msemaji Mkuu wa Serikali yupo katika ziara ya kikazi Mkoani Arusha ambapo atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.