" Nawaagiza viongozi wote wa Wilaya,Halmashauri na wakuu wa idara kwa Mkoa wa Arusha kukagua maeneo yote na kujiridhisha mwenendo mzima wa sensa kabla ya tarehe ya mwisho."
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella alipokuwa akikagua zoezi la sensa ya watu na makazi katika Wilaya ya Longido.
RC Mongella amebaini kuwa kuna baadhi ya maeneo makadirio ya kaya yalikuwa chini au zaidi.
Hivyo amewataka viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote kuyabaini hayo maeneo na kuchukua hatua haraka za kuhakikisha kaya hizo zinahesabiwa.
Lengo la Mkoa sio tu kumaliza zoezi la sensa kwa muda uliopangwa bali kuhakikisha kila kaya inahesabiwa.
Aidha, amewaagiza viongozi wa makarani kuhakikisha wale wanaomaliza kuhesabu katika maeneo yao mapema wapangiwe maeneo mengine ambayo yanauwitaji zaidi ili kaya zote ziweze kufikiwa.
Karani kutoka Wilayani Longido Frida Mchome amesema zoezi la sensa kwa upande wake limeenda vizuri na alifanikiwa kuhesabu kaya 70 na akahamishiwa kwenye eneo jingine.
Frida amesema changamoto kubwa aliyokutana nayo ni baadhi ya watu kutowakuta kwenye kaya kwababu ya majukumu yao ya kikazi hivyo kupelekea kufanya zoezi la sensa hadi usiku.
Samweli Steven ni miongoni mwa wananchi waliohesabiwa na amesema zoezi la sensa ni nzuri kwani litasaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo na amemshukuru Rais Samia kwa kuleta zoezi hilo.
RC Mongella anaendelea na zoezi la kufuatilia mwenendo mzima wa sensa ya watu na makazi katika halmashauri za Mkoa na kutatua changamoto zinazokuwa zimejitokeza katika maeneo hayo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.