“Nitasimamia mazingira ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha yawe mazuri na rafiki kwenu kwa kuyatambua na ikiwezekana kutatua changamoto zenu”.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha,jijini Arusha.
Amewataka wafanyabiashara kutumia ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa karibu sana kwa kuleta changamoto zao kwa uhuru kupitia idara ya Uchumi na Uzalishaji mali.
Aidha, amewashauri wafanyabaishara kuwa na mazoea ya kuchukua mikopo katika mabenki ili iwasaidie kukuza biashara zao kwa kasi sana na kuongeza tija.
Pia, amewasisitiza kuendelea kulipa kodi hata kama kuna changamoto zimejitokeza hasa katika kipindi hiki ambapo dunia ilikubwa na ugonjwa wa Corona, amesema kodi zinasaidia sana kuleta maendeleo yote ambayo yanaonekana kwa sasa katika nchi.
Vile vile amewataka wafanyabiashara wadogo hali maarufu kama (wamachinga) kuzingatia usafi wa mazingira pindi wanapofanya biashara zao kwenye maeneo yao, hii itasaidia kuliweka jiji la Arusha katika mazingira safi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wote mwenyekiti wa chama cha waendeshaji wa shughuli za watalii (TATO) bwana Wilbrod Chambulo, amesema wao wataendelea kushirikiana na serikali kwa karibu zaidi.
Amemuomba Meneja wa Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA) kutenga dirisha maalumu la kuhudumia wafanyakazi waliopunguzwa kazi kwenye makampuni mbalimbali ya Utalii kutokana na janga la Korona ili kuwapunguzia adha ya kukaa katika foleni.
Chambulo amesema, mabenki mengi yamekuwa msaada mkubwa sana kwa wafanyabiashara kwa kutoa mikopo na amewashauri wafanyabiashara wenzake kutumia mabenki kuweka fedha zao badala ya kukaa nazo nyumbani.
Akijibu hoja hizo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania bwana John Mwigulwa amesema, tayari TRA wameandaa dirisha maalumu la kusikiliza mahitaji mbalimbali ya wateja wao hususani wanaotoka katika sekta ya Utalii.
Aidha , amewataka wafanyabiashara kuwa waaminifu katika kipindi hiki ambacho dunia imekubwa na ugonjwa wa Corona kwani wapo baadhi yao wanatoa taarifa za kufunga biashara zao lakini mifumo ya TRA inaonesha bado wanafanyabiashara.
Mheshimiwa Kimanta, amejitambulisha rasmi katika jumuiya ya wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha na kuwaomba kufanya kazi kwa ushirkiano mkubwa na serikali yao ili kuleta maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.