Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella ameziagiza halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kuhakikisha vifaa vyote vinaletwa kwenye vituo vya afya vinawekwa katika maeneo husika na vianze kufanya kazi.
Kauli hiyo ameitoa Wilayani Karatu alipokuwa akipokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya hospitali ya Wilaya vilivyotolewa na benki ya NMB.
Amesema Serikali ya awamu ya sita pamoja na wadau mbalimbali wanatoa fedha vyingi kwa ajili ya kununua vifaa hivyo, amewataka watumiaji kuvitunza ili viweze kutumika kwa muda mrefu.
"Juhudi hizi za Serikali ni katika hatua ya kuhakikisha wananchi wanatatuliwa kero na inawapa uwezo wakujiletea maendeleo yao wenyewe na nchi kwa ujumla".
Vilevile, aitaka halmshauri na Wilaya ya Karatu kuhakikisha huduma zote zinaanza kutolewa mapema ili thamani ya fedha zilizoletwa zinakuwa na tija.
Akitoa shukrani kwa wadau mbalimbali Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba amesema Serikali imetoa jumla ya fedha bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Pia,amewashukuru wananchi waliotoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya Wilaya.
Amesema Wilaya imejipanga kuhakikisha huduma zote zinatolewa ifikapo Agosti, 2023.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu Karia Rajabu amesema tayari majengo 7 yameshakamilika katika hospitali hiyo na ameomba wadau wengine waendelee kujitokeza kuchangia vifaa mbalimbali ili huduma inayotolewa iweze kuwa bora zaidi.
Nae, Afisa Mkuu wateja wakubwa na Serikali kutoka benki ya NMB Alfred Shao amesema, benki hiyo imetoa vifaa vyenye thamani ya Milioni 24 ikiwa imejumuisha Vitanda na Magodoro 20,Mashuka 100, Makabati 20 na Mabenchi 50 kwa ajili ya hospitali hiyo ya Wilaya.
Hospitali ya Wilaya ya Karatu ilianza kujengwa 2021 na kwa sasa imeshaanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na hadi kufikia Agosti 2023 itakuwa imeshakamilika na huduma zote zitatolewa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.