Benki ya NMB leo Mei 22, 2024 imekabidhi Pikipiki 20 kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ili kulisaidia Jeshi la Polisi katika kuimarisha na kustawisha Ulinzi na usalama kwenye Mkoa wa Arusha ulio muhimu na kitovu cha Utalii kwenye Kanda ya Kaskazini mwa Tanzania.
Bw. Filbert Mponzi, Afisa Mkuu wa Biashara na wateja binafsi wa Benki ya NMB Tanzania amesema Benki hiyo inaamini kuwa Usalama Ukiimarika utalii utakua zaidi na hivyo kusaidia kusisimua uchumi wa Arusha na kuongeza pato la Mkoa kupitia sekta hiyo muhimu yenye kuuingizia Mkoa wa Arusha na Nchi fedha nyingi za Kigeni.
Aidha Benki ya NMB imesema imeamua kutoa msaada huo kwa Mkoa wa Arusha kutokana na maono mazuri ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ya kuimarisha ulinzi na usalama Mkoani Arusha pamoja na kukuza utalii ili kuweza kuwanufaisha wakazi wa mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa Mkoa ameishukuru benki ya NMB kwa msaada huo na kuendelea kujitoa kwa jamii ya Arusha, akisema Benki hiyo imeendelea kuwa mfano katika kurudisha kwenye jamii sehemu ya faida wanayoipata.
Ikiwa ni kilele cha utekelezaji wa ahadi yake ya kulipatia Jeshi la Polisi pikipiki 50, Mhe. Paul Christian Makonda pia ameitaka Jamii kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kufichua uhalifu na wahalifu ambao wamekuwa wakitatiza jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Halikadhalika Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda pia amewataka wakazi wa Arusha kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba kwa lengo la kuondoa manung'uniko na pia kutengeneza Nuru njema isiyokuwa na malalamiko pale watakapoufikia Uzee wao ama watakaposhindwa kuzalisha mali kwa ufanisi unaotakiwa.
Benki ya NMB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo Mkoani Arusha ambapo wiki hii pia wanajiandaa kukabidhi meza na madawati kwenye shule za mkoa msingi na Sekondari zilizopo mkoani Arusha zenye thamani ya Shilingi milioni 146 za Kitanzania ili kusaidia katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuweka miundombinu mbalimbali ya kukuza elimu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.