Wadudu aina ya Nzige waliokuwa wamevamia pori Wilayani Longido wamedhibitiwa kwa zaidi ya 70%, baada ya kunyunyuziwa dawa ya kuwauwa.
Nzige hao waliovamia pori la Kijiji cha Kimokouwa na Kijiji cha Sinya wilayani humo wakitokea Nchi jirani ya Kenya, hawakuleta madhara yoyote katika maeneo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Idd Kimanta amekagua eneo la Kimokouwa lililovamiwa na Nzige hao na kujionea njinsi wadudu hau walivyouwawa kwa kupuliziwa dawa.
Kimanta ameishukuru Wizara ya Kilimo, Taasisi ya utafiti wa viwatilifu katika ukanda wa Kitropiki (TPRI),Viongozi wa Wilaya ya Longido na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa waliouwonesha hadi kufanikiwa kuwadhibiti Nzige kwa kiasi kikubwa.
Akitoa taarifa ya namna zoezi la udhibiti Nzige lilivyokuwa kwa Mkuu wa Mkoa,bwana Oshingi Shila mtalaamu kutoka TPRI amesema, Nzige hao walifika katika Kijiji cha Oriendeki na kundi la pili lilifika katika Kijiji cha Kimokouwa na kwenda hadi Kijiji cha Sinya.
Bwana Oshingi ameeleza kuwa Nzige hao hawajaleta madhara yoyote kwani walikuwa bado kwenye hatua za ukuaji hivyo hawakuwa na nguvu ya kuharibu mazao katika eneo hilo.
Amesema zoezi la kuwauwa lilifanyika kwa kunyunyuzia dawa kwa ndege kwa kushirikiana na shirika la Chakula Duniani (FAO) na kufanikiwa kuwadhibiti kwa zaidi ya asilimia 70 na bado wataalamu wanaendelea kulifuatilia eneo hilo ili kujiridhisha kama Nzige wote wamedhibitiwa.
Bwana Daudi Saloon ni mwananchi wa Kijiji cha Kimokouwa amesema kuwa Nzige hao walivamia pori la Kijiji hicho na anasema Nzige hao walikuwa wengi sana lakini Serikali imefanikiwa kuwadhibiti kwa kiasi kikubwa sana.
Wadudu aina ya Nzige waliingia Wilayani Longido Februari 20,2021 kutokea nchi ya Kenya na mnamo Februari 23 Serikali ilifanikiwa kuwadhibiti kwa kuwanyunyuzia dawa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.