Na Elinipa Lupembe.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Arusha, Komred Loy Ole Sabaya, akizungumza kwenye mkutano wa hafla fupi ya ugawaji wa magari ya Afya, kwa mikoa ya Arusha na Manyara, kwenye ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, leo 13 Desemba, 2023.
Ole Sabaya, ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na hadhara ya Watumishi wa Umma, tangu kuchaguliwa kushika nafasi hiyo, ametumia wasaa huo kuwashukuru na kuwapongeza, watalamu kwa kazi nzuri ya usimamizi na utekelezaji wa shughuli za maendeleo za mkoa wa Arusha,kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya hadi mkoa.
Amesema kuwa, wananchi kwa sasa, wanashuhudia kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, maendeleo yamefika kila kona huku wananchi wakiendelea kunufaika na miradi iliyojengwa kwenye maeneo yao
Aidha amewashukuru viongozi wa Chama na Serikali pamoja na watalamu kwa ushirikiano mkubwa baina yao, unaosababisha amani na utulivu katika mkoa wa Arusha kwa sasa, jambo linalosababisha wanaArusha kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali na sio migogoro.
"Ninakupongeza sana Mkuu wa mkoa, Mhe. Mongella, umekuwa kiongozi mwadilifu mwenye kuunganisha watu unaowaongoza, umekuwa kiungo kati ya viongozi wa Chama, Serikali na wananchi pia, tuendelee kushikamana ili kuwahudumia wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, chama ambacho ndio kimeshika dola kwa sasa". Amesisitiza Ole Sabaya
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo, ameweka wazi kuwa, katika mkoa huo, bado kuna changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara, jambo linalosababisha kero kwa wananchi kwa baadhi ya maeneo na kumuomba Mhe. Waziri OR- TAMISEMI, kupitia Wakala wa barabara TARURA, kuongeza nguvu katika matengenezo ya barabara pamoja na ukamilishaji wa miradi viporo ya barabara.
"Mhe. Waziri nikuombe utusaidie kufanya matengenezo ya barabara ambazo hazipitiki lakini zaidi kukamilisha miradi ambayo iko kwenye utekelezaji, yapo maeneo ambayo bado hayapitiki na kusababisha kero kwa wananchi, tunaomba utusaidie kutatua ama kupunguza changamoto hii". Amesisitiza Mwenyekiti huyo
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.