Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amewaagiza wakurugenzi na Maafisa elimu Mkoa wa Arusha kuhakikisha ufaulu unaongezeka katika shule zote za Msingi.
Maelekezo hayo ameyatoa alipokuwa akizindua miradi mbalimbali katika shule ya msingi Endabash wilayani Karatu, miradi iliyofadhiriwa na shirika la World Vision Tanzania.
Amesema ni aibu kubwa kwa shule kama ile kupata majengo mazuri ya Madarasa,Ofisi ya walimu, Madawati na Vyoo alafu ufaulu uwe chini kwani kwa mwaka jana 2020 ulikuwa 67%.
Kimanta amesema mwaka jana 2020 ufaulu wa Mkoa kwa shule za msingi ulikuwa 92.4%, hivyo kwa mwaka huu 2021 anataka kila shule ifaulishe si chini ya 90% ili kurudisha fadhila zinazotolewa na wafadhili hao na kuendelea kuwatia moyo ili waongeze miradi mingine mingi.
Hata hivyo, Kimanta amewasisitiza wazazi kutoa ushirikiano katika juhudi hizo kwa kusimamia mahudhuria ya Watoto wao kwa kuwahimiza kuhudhuria shule kila mara.
Pia, amewataka wananchi wa Kijiji cha Endabash kuwaunga mkono wadau hao wa maendeleo kwa kujenga bwalo la chakula kwani shule hiyo haina bwalo la chakula ambalo inaleta usumbufu kwa Watoto kukosa sehemu ya kupatia chakula hasa katika kipindi cha mvua.
Nae,Kaimu Mkurugenzi wa Mradi kutoka World Vison bwana Victor Kasabala, amesema shirika hilo limekuwa likifanya kazi katika Mikoa takribani 16 hapa Tanzania na wamejikita katika sekta mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Maji na kukuza ufahamu kwa wasichana.
Amesema, shirika hilo limeweza kutekeleza miradi yake kwa urahisi kutokana na mazingira mazuri yalipo ya Amani na Utulivyo yaliyotengenezwa na Serikali ya Tanzania.
Meneja Mradi kutoka World Vision bwana Goodluck Nnko amesema, mradi huo ulikuwa wa kujenga Madarasa 10, jengo moja la utawala, Matundu ya Vyoo 18, Madawati 66, Masinki vituo 3 na Jiko.
Mradi huo ilianza July 2020 na umekamilika Aprili 2021 na jumla ya Shilingi Milioni 558 zimetumika katika mradi huo.
Bwana Nnko amesema, World Vision wanaendelea kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo kwenye nyanja mbalimbali kama vile sekta ya Maji, Afya na Elimu.
Shirika la World Vision Tanzania limekabidhi jumla ya miradi 7 kwa Serikali baada ya kukamilika katika shule ya msingi Endabash na wanaendelea kusimamia miradi mingine katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.