Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amezitaka Kamati za Lishe Mawilayani kuhakikisha zinakwenda Vijijini kufundisha na kuhamasisha masuala ya Lishe kwa Jamii.
Amesema hayo aliopokuwa akiongoza Kikao cha Lishe Mkoa wa Arusha kikichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati wakijadili mpango mkakati wa namna ya kukabiliana na changamoto ya Lishe duni katika Jamii hususan kwa siku 1000 za mtoto tangu azaliwe.
Amesema kuwa suala la Lishe halina mjadala wala mbadala na kuwa Lishe bora ndiyo inayopelekea kupata nguvu kazi iliyobora na Viongozi bora, Viongozi bora huzaa Taifa imara,hivyo kucheza na masuala ya Lishe ni kuhujumu mipango ya maendeleo ya Taifa kitu ambacho ni hatari kwani hupelekea Taifa kuwa na idadi kubwa ya Watu wenye udumavu.
Katika kuhakikisha suala la Lishe linapewa kipaumbele, Mongella ameziagiza Kamati za Lishe kufanye ziara Vijijini kwaajili ya kwenda kutoa Elimu na hamasa kwa Jamii ili kuwapa uelewa mpana wa faida za Lishe kwa mama mjamzito na Watoto chini ya Miaka 5 kwani kila Halmashauri ilishagizwa kutenga fedha za kuchangia mpango Lishe kwa mtoto mchanga.
"Nawaombeani Wakuu wa Wilaya mkazisimamie Kamati za Lishe ili ziweze kutoa elimu ya Lishe kwenye Kaya hii itasaidia Jamii kupata uelewa wa umuhimu kwa mama mjamzito na kwa siku 1000 za mtoto toka azaliwe" Alisema Mongella.
Sambamba na hilo, Mongella amesema ni vyema Ofisi za Waganga wa Wakuu wa Wilaya wakateuwa timu ya Maafisa uhamasishaji Lishe wenye waliobobea katika eneo hilo na ambao wanatambua malengo na mikakati ya Taifa kuhusu Lishe kwani kwa kutofanya hivyo zoezi la Lishe litakuwa bure.
"Tunapofika kwenye suala la uelemishaji nawaomba saana Waganga Wakuu wa Wilaya lazima tupeleke Maafisa Lishe wanajua kusoma vizuri Scorecard ya Lishe ili watusaidie kutoa elimu na kutupa takwimu sahihi za hali ya Lishe kwenye Wilaya zetu" Alisema Mongella.
Kikao hicho cha Lishe Mkoa kilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi pamoja na Wataalam wa Lishe toka Wilaya zote za Mkoa wa Arusha ambapo kila Wilaya iliwasilisha taarifa zake za utekelezaji na mikakati ya kukabiliana na changamoto za Lishe katika Jamii.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.