POLISI WAPATIWA MBINU KUKABILIANA NA MAUAJI YA WANYAMAPORI BARABARANI.
Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Longido Mkoani Arusha leo wamekutanishwa na wadau wa wanyamapori kufundishwa na kujadili kwa pamoja namna bora ya kukabiliana na mauaji ya wanyamapori kwa kugongwa na vyombo vya moto barabarani.
Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Peter Lusesa amesema kutokana umuhimu wa sekta ya Utalii, Jeshi la Polisi lilianzisha mradi unaojulikana ‘Utalii Salama’ ambapo wanyamapori ni mhimili wa sekta hiyo hivyo wanalojukumu la kuhakikisha usalama wa wanyama hao unakuwepo wakati wote.
ACP Lusesa amewataka Askari hao ambao ni Wakaguzi kata pamoja na wale wa usalama barabarani kutumia Mradi huo kwenda kukutana na madereva pamoja na wananchi kwa ajili ya kuwapa elimu juu ya madhara ya kugonga wanyamapori hao lakini pia kuwaeleza faida ipatikanayo kupitia utalii.
Naye Afisa Ikolojia na Utafiti toka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya OIKOS Afrika Mashariki Bi. Eliengerasia Koka amebainisha wameamua kuandaa semina hiyo mahususi kwa ajili ya Askari hususani wale wa kata ili waende kuwaelimisha wananchi kuhusiana na madhara ya kuua au kugonga wanyamapori na faida zao.
Afisa huyo amesema taasisi hiyo imebaini kuwa wanyamapori wengi wanakufa kwa kugongwa na magari barabarani hususani katika barabara ya Arusha Namanga na hata zile zinazopita katika vijiji mbalimbali katika wilaya hiyo, hivyo kupitia semina hiyo Askari kata hao watapata maarifa zaidi ya kwenda kuwaelimisha wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Longido Mrakibu wa Polisi SP Juma Bonza amesema endapo wananchi watapewa elimu ya kutosha, kuweka alama za barabarani katika maeneo yenye wanyama wengi pamoja na kuchukua hatua kwa madereva watakaokiuka Sheria itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo.
Naye Mkaguzi Kata ya Namanga Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Zainabu Sengasu amesema elimu waliyoipata wataenda kuifikisha kwa wananchi ambapo amewaomba wadau kufadhili mabonanza kama vile michezo ambayo hukutanisha watu wengi katika kata zao hali ambayo itasaidia kufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.