Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Mhe. Profesa Kitila Mkumbo amemsifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa ubunifu na kasi aliyonayo katika kutekeleza maono na mipango ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kuna suala la uongozi kuwa na cheo,na wenye vyeo tupo wengi ila unakifanyia nini cheo ni jambo jingine kabisa ambalo mdogo wangu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda unakifanyia haki cheo chako. Ni mbunifu na kila sikua hapa Arusha kuna kitu kipya" amesema Profesa Mkumbo.
Waziri Mkumbo pia amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa uratibu wa Kambi ya matibabu iliyomalizika hivi karibuni akisema imekuwa na mafanikio makubwa na imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi ambao walikuwa hawajafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa.
"Nilikuwa namtania leo asubuhi nikamwambia ujue wenzako tukikutana wengi wanazungumzia tu Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa lakini wewe mwenzangu unazungumzia biashara, viwanda, uwekezaji.Nikamuuliza na wewe ni mwenyekiti wa kamati ya usalama?", Ameongeza Mhe. Kitila Mkumbo.
Waziri Prof. Kitila aliyeambatana na Maafisa mbalimbali wa wizara na Kituo cha TIC nchini Tanzania, alikuwa akifungua Kituo cha uwekezaji TIC kanda ya Kaskazini, Kituo ambacho kimehamishwa kutoka Mkoani Kilimanjaro kwenda Mkoani Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.