Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Misseile Albano Musa, ametembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kiutu, halmashauri ya Arusha, mradi unaotekelezwa na serikali kupitia program ya kuboresha elimu ya sekondari nchini (SEQUIP).
Katibu Tawala huyo, ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza mradi huo kwa viwango ambavyo ubora wa mradi unaonekana hata kwa macho licha ya kwamba mradi huo bado haujakamilika.
"Ninawapongeza wataalamu wa halmashauri ya Arusha, inaonesha namna gani mnafanyakazi kama timu, endeleeni kufanya hivyo ili kufikia malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi". Amesisitiza Katibu Tawala huyo.
Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wanafunzi wa kidato cha kwanza wapangiwe shule hiyo na kuanza masomo ifikapo Januari 2023.
Awali akisoma Taarifa ya mradi huo, kwa niaba ya msimamizi wa mardi huo, na Makamu mkuu wa shule ya sekondari Kiutu, Mwl. Upendo Mollel, amesema kuwa mpaka sasa mradi umefikia asilimia 65 kukamilika na makadirio ya gharama za ukamilishaji wa mradi huo ni takribani shilingi milioni 250 fedha ambazo zikipatikana mradi utakamilika mpaka mwisho.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amemshukuru Katibu Tawala huyo kwa kutembelea mradi huo na halmashauri yake kwa ujumla, na kuahidi kutekeleza maagizo, yote aliyoyatoa lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapangiwa na kuanza masomo mapema mwezi Januari 2023.
Awali Afisa Elimu sekondari, halmashauri ya arusha, Mwl. Menard Lupenza amesema kuwa, Serikali kupitia program ya SEQUIP ilitoa kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kiutu, ujenzi unaojumuisha jengo la ghorofa mbili lenye kubeba vyumba 8 vya madarasa, maktaba, maabara za masomo ya TEHAMA na vyoo vya wanafunzi, jengo la Utawala na Maabara za masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.