Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Albano Musa ameagiza uongozi wa halmashauri ya Jiji la Arusha kujibu hoja kumi za mwaka wa fedha uliopita ikiwemo deni la shilingi bilioni 3.55 pamoja na mapato ya halmashauri hiyo shilingi bilioni 2.1 ambayo hayajakusanywa kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Katibu Tawala huyo , amesema hayo katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23, ulofanyika kwenye ukumbi wa Mkutano wa halmashauri hiyo mapema leo Juni 15, 2024.
Amesema kuwa, mwaka ujao wa fedha Mkoa wa Arusha utakuwa bega kwa bega kuhakikikisha inafuatilia miradi yote na ukusanyaji wa mapato kwa Jiji la Arusha na kuagiza kuacha tabia ya kumwachia muweka hazina kujibu hoja peke yake bali kila mhusika ajibu hoja na kuzijua ikiwemo viambatanisho
Hata hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha, Mhandisi, Juma Hamsini amesema kuwa, halmashauri hiyo imepata hati isiyo na shaka kwa mwaka wa fedha 2022/23 ikiwemo kutekeleza hoja 23 kati ya 49, ambapo hoja 23 zimetekelezwa na kubaki na hoja 26 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
"Lazima madeni ya nyuma yakusanywe lakini pia tutasimamia ulipaji wa madeni kwa kutumia POS ili kuhakikisha madeni ya nyuma yote yanakusanywa lakini pia tutaboresha mifumo ya ukusanyaji kodi ili kuhakikisha fedha na miradi iliyopangwa inakamilika kwa wakati" amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Felician Mtahengerwa amesisitiza watumishi kupunguza hoja zilizopo na hatimaye Jiji la Arusha kupata hati safi na kutumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wote wa halmashauri hiyo kwa ushirikiano wao unaopelekea Jiji hilo kupata hati safi .
Awali, Diwani kata ya Sokoni I , Saruni Olodi ameomba mawakala wa ukusanyaji taka Jiji la Arusha wanaodaiwa kiasi cha shilingi milioni 14,466,300 kupitia mashine za POS warudishe fedha hizo kwani hadi sasa shilingi 14,466,300 pekee ndio zimelipwa kama deni.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.