Na Elinipa Lupembe
Katibu Tawala mkoa wa Arusha Massaile Albano Musa amewafunda watumishi wa halmashauri ya Meru kwa kuwaagiza kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu katika kuwahudumia wananchi kwa kuepuka vitendo vilivyo kinyume na maadili ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita.
Katibu Massaile amezungumza na watumishi hao, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za watumishi, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo ya Meru.
Amesema kuwa watumishi wa Umma ndio injini ya serikali, wanaotegemewa kufanya kazi walizokasimiwa za kutoa huduma bora kwa wananchi kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania hivyo kila mtu kwa nafasi na taaluma yake anatakiwa kutimiza wajibu wake.
"Niwapongeze watumishi wa halmashauri ya Meru kwa kazi nzuri, mnafanya kazi nzuri na zinaonekana ingawa bado kuna maeneo ambayo bado hamjafikia malengo, niwasihi muongeze bidii kwa kujipanga upya kwa kufanya kazi kama timu kwa kuheshimiana na kupendana kila mmoja kumthami mwenzake"
Aidha amewakanya watumishi hao kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu, vitendo ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa Umma na kuvitaja vitendo hivyo kuwa ni rushwa, majungu, ulevi na aina zote za vitendo viovu.
Hata hivyo watumishi wa halmashauri ya Meru licha ya kuupongeza uongozi wa halmashauri yao na mkoa kwa kutatua kero za watumishi kwa asilimia kubwa sasa tofauti na miaka ya nyuma.
Afisa Mkaguzi wa Ndani CPA. Wamilika Mlangi ameweka wazi kuwa, sio kwamba watumishi hawana kero ila kwa sasa kero zao zinafanyiwa kazi na kutatuliwa kwa wakati jambo ambalo linawapa ari ya kufanya kazi kwa bidii.
"Tukisema hatuna kero, tutakuwa waongo, kero tunazo lakini viongozi wetu wa halmashauri wanazitatua kwa wakati, binafsi nilikuwa na changamoto ya kubadilishiwa muundo tangu mwaka 2012 lakini kwa sasa iko sehemu nzuri inashughulikiwa" Amesema CPA Wamilika
#KaziInaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.