Na Elinipa Lupembe.
Maadhimisho ya sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi kitaifa mwaka 2024, yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha huku maandalizi ya awali yakifanyika na tayari vikao vya awali vilivyoikutanisha kamati tendaji vikifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Akizungumza kwenye vikao hivyo, Rais wa TUKTA, Nyamhokya Tumaini, amesema kuwa mkoa wa Arusha umeteuliwa kufanyika sherehe za Wafanyakazi Kitaifa mwaka 2024, huku Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,akiridhia kuwa mgeni rasmi na wakiamini sherehe hizo kufana na kufanyika kwa mafanikio makubwa, kwa maslahi mapana ya wafanyakazi na Taifa kwa ujumla wake.
Rais huyo, ameeleza umuhimu wa kuadhimisha sherehe za Mei Mosi kuwa, ni pamoja na kutambua mchango wa wafanyakazi katika jamii, kusherehekea haki za wafanyakazi, mafanikio yao, na kusisitiza umuhimu wa haki na wajibu katika kazi.
Naye Mwenyekiti wa vikao hivyo na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, ameshukuru kwa kuchagua mkoa huo kupewa dhamana ya kuandaa na kufanyika maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa, sherehe ambazo ni muhimu kwa Taifa, kwa kuwa wafanyakazi ndio injini ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa la Tanzani.
Mhe.Mongella amesisistiza kuwa, Serikali inatambua na kuthamini sikukuu hiyo muhimu kwa wafanyakazi kwa kuwa, wafanyakazi ndio msingi wa kuendesha shughuli zote za Serikali na ndio kiwanda kinachozalisha matunda ya maendeleo ya nchi yetu na dunia nzima.
Aidha amechukua nafasi hiyo kuwakaribisha Arusha kwa niaba ya wanaArusha wote na kuahidi kusimamia vema maandalizi yote mpaka kilele cha siku hiyo kwa kushirikiana bega kwa bega na timu ya maandalizi ili kuhakikisha Maadhimisho mkoa wa Arusha yanakuwa ya kipekee yenye kuleta tija na mafanikio makubwa kwa wafanyakazi na Taifa pia .
Awali, sherehe za Wafanyakazi Mei Mosi huadhimishwa tarehe 01 Mei kila mwaka na mwaka 2024 zinategemewa kufanyika kitaifa mkoani Arusha
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.