Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta amemuwakikishia Profesa Hilonga kuwa atahakikisha kila shule hususani za vijijini zinapata mtambo wa kuchuja maji kwa ajili ya matumizi mashuleni.
Ameyasema hayo alipokuwa akizindua mradi wa kutengeneza mtambo wa kusafisha maji safi na salama wa kampuni ya Gongali Model iliyopo jijini Arusha.
Kimanta amesema,kutokana na jamii nyingi kutumia maji yasiyo safi na salama kwa Mkoa wa Arusha,mtambo huo unaojulikana kama “nano filters”,utasaidia upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema, amefurahishwa na uwazishwaji wa mtambo huo kwani umeweza kutoa ajira kwa watu kwa kujipatia kazi ya kuuza maji katika maeneo mbalimbali.
Nae, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Gongali Model Profesa Askawar Hilonga amesema, mtambo huo wa kuchuja maji umeweza kuajiri vijana takribani 127 na kuhudumia watu zaidi ya 300,000.
Amesema lengo kubwa la mradi huo ni kuwafanya vijana watumie elimu zao katika kujiajiri hususani kwa kutatua changamoto zilizopo katika jamii zao.
Pia, kuhakikisha jamii ya Arusha inatumia maji yasiyo na madini ya floride ili kulinda afya za wananchi kwani maji yanayopatikana katika Mkoa huo yana kiasi kikubwa cha madini hayo.
Amesema mbali na mtambo huo kuchuja maji pia unapunguza kiwango cha madini ya Floride katika maji.
Mradi wa Nano filters mpaka sasa umeshasambaa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha kwa lengo la kupunguza gharama za upatikanaji wa maji safi na salama.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.