Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Ceylex Engineering (Pvt) Ltd, aliyepewa kandarasi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vya mkoa wa Arusha, mradi wenye thamani ya shilingi Bilioni 78.8, kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa wakati ili kufikia lengo la Serikali ya awamu ya sita la kuhakikisha nchi nzima inakuwa na umeme wa uhakika.
Mhe. Makonda ametoa rai hiyo, wakati akimkabidhi Mkandarasi tenda ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 186 vinavyopatikana kwenye halmashauri zote saba za Mkoa wa Arusha, mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye soko la Kikatiti wilaya ya Arumeru, na kuzindua kandarasi hiyo kwenye kitongoji cha Kambi ya Mkaa wilayani Arumeru mkoani Arusha leo Septemba 26, 2024.
Hata hivyo Mhe Makonda ametumia fursa hiyo Kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo akiahidi kusimamia ipasavyo ukamilishaji wa miradi na usimamizi wa fedha zote za miradi ya maendeleo zinazoletwa mkoani Arusha.
"Nishati ni chagizo muhimu sana kwenye Taifa linalotaka kuendelea, hamuwezi kuendelea bila umeme na gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa kutokana na gharama za nishati. Kama upatikanaji wa umeme ni wa uhakika na wa nafuu unawezesha wananchi wengi zaidi kufanya shughuli zao."Amesema Mhe. Makonda.
Hata hivyo, licha ya kuwataka wakazi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kuitunza amani ya Tanzania, Mhe. Makonda pia amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha kuwa anawatumia vijana wa maeneo husika katika kutekeleza shughuli za mradi huo ili nao waweze kunufaika kiuchumi katika utekelezaji wake.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.