Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametumia jukwaa la maadhimisho ya siku ya maridhiano leo Jumatano Februari 26, 2025, kumualika Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, kuhudhuria siku ya Nyama choma Mkoa wa Arusha itakayofanyika Machi 07, 2025, siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Kitaifa yatafanyika Mkoani Arusha kwenye viwanja vya Michezo vya Sheikh Amri Abeid, mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye bara la Afrika na dunia inamtambua kama Kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Makonda amemueleza Waziri Mkuu ambaye amekuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye maadhimisho ya siku ya maridhiano, kuwa siku hiyo ya nyama choma itakuwa na nia ya kuonesha jamii umuhimu wa matumizi ya nishati safi na namna ambavyo nishati hiyo inaweza kutumika mpaka kwenye uchomaji wa nyama tofauti na ambavyo watu wengi wanaamini kwenye mkaa na kuni kama nishati sahihi katika uchomaji wa nyama.
Mhe. Makonda amewaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kuwa kufikia leo tayari Mkoa umeandaa ng'ombe 360, Kondoo na mbuzi 170 pamoja na wanyamapori aina mbalimbali ikiwemo swala, Nyati na pofu, ambao wote watachinjwa na kuliwa bure na wakazi wa Arusha na wageni mbalimbali watakaokuwa Arusha kusherehekea mafanikio ya wanawake hapo Machi 08, 2025.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.