Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi wakati akijibu hoja na kero mbalimbali za wananchi wa Arusha, ametangaza ujio wa ziara ya Kata zote za Mkoa wa Arusha ikiwa ni maelekezo na maagizo ya Chama Cha Mapinduzi.
Mhe. Makonda ametangaza ujio wa Ziara hiyo mapema leo Juni 04, 2024 wakati alipokuwa akijibu baadhi ya hoja na changamoto zilizoibuliwa na wananchi wa Kata ya Usa River wilayani Arumeru, wakati Katibu Mkuu wa CCM alipopita kusalimia na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo, wakati akiwa njiani kuelekea Mkoani Kilimanjaro kuendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kusikiliza wananchi wenye kero mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa amemwambia Katibu Mkuu wa CCM Taifa kuwa moja ya changamoto kubwa aliyopanga kwenda kuitafutia ufumbuzi ni mgogoro wa ardhi unaohusisha vijiji vitatu vya Maloloni, Kwaugolo na Velenska ambao wamekuwa na mgogoro na ardhi ambayo mwanzoni ilikuwa ikimilikiwa na Chama cha Ushirika kabla ya kutwaliwa na serikali na baadae kurudishwa kwa wananchi waliotakiwa kuendeleza eneo hilo na kujiamulia matumizi yake.
Akijibu baadhi ya changamoto nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha amewaambia wakazi wa Usa River kuwa huduma ya Maji katika eneo hilo inashughulikiwa na Mamlaka ya Maji inahakikisha kuwa eneo hilo linakuwa na usambazaji mkubwa wa maji kwani tayari vipo vyanzo kadhaa vya maji vinavyozalisha Maji kupeleka Arusha Mjini.
Aidha Mkuu wa Mkoa pia amemuambia Balozi Dkt. Nchimbi kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Arumeru tayari imeanza mchakato wa ujenzi wa kituo cha mabasi kwenye eneo hilo pamoja na soko la wafanyabiashara kutokana na eneo hilo kukosa huduma hizo kwa muda mrefu hivi sasa.
Mkuu wa Mkoa mwishoni mwa mwezi Mei kwa siku sita, alifanya ziara ya Kikazi kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Arusha ambapo kero za wananchi zaidi ya 3000 zilitatuliwa huku wengine wengi wakipata misaada ya kisheria kutoka kwa Chama cha wanasheria wa Tanganyika - TLS pamoja na misaada mingine binafsi ya kifedha, vitendeakazi, Baiskeli za walemavu pamoja na bima za afya kwa watoto.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.