Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amekutana na wadau wa sekta ya Utalii mkoa wa Arusha na hatimaye kuunda Timu Maalum, itakayokwenda kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa ujumla wake.
Mhe. Makonda ameunda timu hiyo mapema leo alipozungumza na wadau hao kwenye kikao, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano ofisi ya mkuu wa mkoa huo, timu inayojumuisha wadau wa sekta hiyo na Watalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha.
Mhe. Makonda ameiagiza timu hiyo kufanya kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja na kuja na maoni na ushauri wa namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa sekta hiyo ikiwemo ulipaji wa tozo za serikali na mapato ya Halmashauri.
Amefafanua kuwa lengo la Serikali ya awamu ya Sita inyoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutengeneza mazingira rafiki kwa wadau na wafanyabiashara wote, waweza kulipa kodi za Serikali bila shuruti na kuendelea kufanya shughuli zao za Kiutalii katika mazingira mazuri.
Hata hivyo, ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Arusha kutumia mifumo ya Serikali katika ukusanyaji wa Mapato ya Serikali ili kupunguza migogoro na wafanyabiashara hao, sambamba na kupunguza gharama za kutumia magari ya Serikali kwenda kukusanya mapato.
“Nendeni sasa mkajikite kutumia mifumo ya kidigitali ambayo imeundwa kurahisisha shughuli za ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kuondoa mianya ya rushwa na kupunguza Migogoro na wafanyabiashara.” Amesisitiza Mhe. Makonda.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha watalii Tanzania, Wilbert Chambulo, amezitaja changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ulipaji wa mapato ya halmashauri, hali inayokatisha tamaa ya kuendelea kufanya shughuli zao na wakati mwingine kupelekea uwepo wa mianya ya rushwa kwa baadhi ya wadau.
Naye, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mhandisi Juma Hamsini, ameahidi kushirikiana na wadau hao kuunda timu hiyo na kushulikia changamoto hizo ndani ya Mwezi Aprili.
Awali, kikao hicho kuwakutanisha pamoja wadau wa sekta ya Utalii na Wataalam wa sekta zote za Umma za mkoa wa Arusha, kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zinazoikabili sekta hiyo
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.