Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Paul Makonda ameweka wazi kuwa, dhamira yake kubwa mkoani Arusha ni kuona kila mwananchi mkoani humo, ananufaika kupitia fursa ya Utalii unaofanyika Arusha.
Akizungumza na wananchi na wanachuo wa Chuo cha Ualimu Patandi pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Elimu Maalum Patandi, muda mfupi baada ya kukamilisha zoezi la upandaji wa miti kwenye viwanja vya chuo hicho, Mhe. Makonda ametamani uchumi wa mwananchi mmoja kuongezeka kupitia fursa na utajiri wa rasilimali ardhi iliyopo Arusha
"Ninatamani kuona kila mwananchi wa Arusha, ananufaika na mzunguko wa fedha unaotokana na sekta nyeti za madini na utalii pamoja na fursa nyingine zilizopo mkoani Arusha, utajiri wa rasilimali hizi umnufaishe kila mwanaarusha".Amesema RC Makonda
Hata hivyo, amewasisitiza wakazi wa Arusha kutambua kuwa mkoa wa Arusha ndio mkoa kinara unaozalisha fedha za kigeni nchini, hivyo kila mwanaarusha anapaswa kuhakikisha ananufaika na pato hilo la mkoa kwa kujikita katika shughuli za uzalishaji na sio kubweteka na kuacha watu wengine kunufaika nazo
Amewataka wananchi hususani vijana ili kuhakikisha kuwa Arusha inaendelea kuwa kinara kwa kuingiza fedha za kigeni kupitia Utalii amewasisitiza vijana kuchangamkia fursa ya utalii kwa kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa, jambo ambalo linasababisha vijana wengi kuwa tegemezi wakati wakisubiri kuajiriwa.
"Hakikisheni tunanufaika na fedha zinazotokana na utalii katika maeneo yetu, hakuna maana ya kijana kusoma vizuri na kurudi nyumbani kukaa, Mkoa wetu unafursa nyingi changamkieni kila mmoja kwa nafasi yake, zipo kazi nyingi zinahitaji rasilimali watu hata kwa ambao hawajapata fursa ya kusoma" Amesisitiza Mhe.Makonda.
Awali, Mkuu wa Mkoa huyo ameataka wakazi wa Arusha, kila mmoja kupanda miti ili kutunza mazingira na kuhifadhi uoto wa asili ambao ni urithi wa thamani kubwa kutoka kwa Mwenyenzi Mungu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.