Na Elinipa Lupembe
Kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024, Mkuu wa mka wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewaasa wananchi wa mkoa huo, kuwakataa viongozi wanato rushwa ili wachaguliwe na kuwasisitiza wasifanye kosa hilo, kwa kuwa rushwa ni adui wa haki, lakini rushwa ni kinyume na mapenzi ya Mungu.
Mhe. Makonda ametoa rai hiyo, kwenye kijiji cha Tukusi kata ya Loksale wilaya ya Monduli wakati akizindua Mradi wa uchimbaji visima 30 vya maji mkoa huo na kuwasisitiza wananchi waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura ya kuwachagua wenyeviti watakao waongoza kwa miaka mitano ijayo.
"Ukimchagua kiongozi aliyekupa rushwa, hutathubutu kumuhoji kwa jambo lolote kwa kuwa tayari ameshakulipa, umeuza uhuru wako wa miaka mitano kwa shilingi elfu 10 na hata maendeleo yakikosekana utalazimika kukaa kimya". Amesema.
Amewahimiza kuwakataa viongozi wanaotaka kuwa madarakani kupitia fedha na vizawadi ambavyo, havina thamani ya kura wanayoitoa, badala yake kuwachagua viongozi waadilifu, wazalendo na wenye uchungu na wenye mipangp ya maendeleo ya kijiji na vitongoji vyao.
Amewasisitiza kutambua kuwa kupitia Uchaguzi, Serikali imewapa nafasi ya kuwaweka viongozi wanaokwenda kuunda Serikali, hivyo Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anataka mwananchi wamsaidie kupata viongozi waadilifu ili waweze kushiriki katika kusimamia vema fedha za maendeleo, wawe sehemu ya kushiriki usimamizi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
"Migogoro ya mingi ndani ya vijiji, mitaa na vitongoji ikiwemo migogoro sugu ya ardhi na haiwezi kuisha kama tukiwachagua viongozi ambao wametoa rushwa, kiongozi anayetoa rushwa, anataka kurudisha pesa aliyokupa, msikubali kuhongwa na mgombea yoyote, utashindwa kumhoji, utakaa kimya mnapodhulimiwa, mnapokosa barabara, jitafakarini kwa nini tunafedhehesha heshima tuliyopewa na Serikali yetu kwa shilingi elfu 10". Amesema Mhe. Makonda
Hata hivyo, amewaasa wagombea wa vyama vyote, wasikubali kutoa rushwa ili wachaguliwe, kwa kufanya hivyo, watajitenga na Mungu, baraka za Mungu zitaondoka na kuwataka kutambua dhamana kubwa wanayopewa na wananchi inahitaji uadilifu wa hali ya juu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.