Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa wamekubaliana kushirikiana pamoja katika kukuza na kuimarisha bunifu mbalimbali za kiteknolojia Mkoani Arusha kama sehemu ya kutekeleza kwa vitendo adhma ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa kidigitali nchini Tanzania.
Wakati wa mazungumzo yao Jijini Arusha leo Machi 12, 2025 ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Waziri Silaa Mkoani hapa, Waziri Silaa ameeleza kuwa serikali pia ipo kwenye utungaji wa sera itakayosimamia bunifu na kampuni changa nchini (startup’s policy) katika kuhakikisha kuwa Vijana wa Arusha na mikoa mingine ya Tanzania wananufaika na bunifu zao mbalimbali za kiteknolojia.
Katika maelezo yake Mhe. Makonda ameahidi kushirikiana na Wizara hiyo katika mchakato huo, akisema Mkoa pia unajiandaa na ujio wa shindano la kushindanisha bunifu za kiteknolojia kwa vijana wa Arusha na amemuomba Waziri Silaa kuitikia wito wa kuhudhuria mashindano hayo pale muda utakapokuwa umefika.
Mhe. Makonda ametumia fursa hiyo pia kusisitiza nia ya Vijana walioaminiwa na Rais Samia kuendelea kushirikiana vyema katika kumsaidia majukumu, akiishukuru Wizara hiyo kwa umarishaji wa miundombinu mbalimbali ya Tehama mkoani Arusha ikiwemo ufungaji wa minara ya simu kwenye maeneo ya Loliondo na Monduli na hivyo kuimarisha huduma za mawasiliano na kusisimua uchumi kwa kurahisisha ufanyaji biashara na kupunguza urasimu kwenye shughuli mbalimbali.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.