"Mkatengeneze timu za ushindi na mzijengee uwezo katika ngazi ya Wilaya na Halmshauri ili utekelezaji wa kazi uwe mwepesi".
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akifunga kikao kazi (Retreat) kwa ngazi ya Mkoa, Wilayani Karatu.
Amesema kikao hicho kilikuwa na mfunzo mbalimbali ikiwemo usimamizi mzuri wa rasilimali watu na mifumo iliyopo Serikalini.
"Retreat kazi yake nikukumbushana mambo muhimu yanasaidia kufanya Mkoa wetu uwe na dira inayoeleweka na itakayotoa matokeo chanya", alisema Mongella.
Niwaombe mkasimamie mifumo vizuri hasa ya ukusanyaji mapato katika Halmshauri zenu na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato.
Aidha, Mongella katika hotuba yake amewasisitiza viongozi wa Wilaya na Halmashauri kwenda kusimamia miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora.
Amesema mafunzo waliyopatiwa yamewasaidia kujitafakari wao kama viongozi na kufahamu walipotoka na waendapo.
Nae, Katibu wa CCM Mkoa Musa Matoroka amesema amefurahishwa na mafunzo hayo na amependekeza mafunzo hayo yapelekwe ngazi za chini hadi kwa wenyeviti wa Vijiji ili nao waweze kujengewa uwelewa utakaowasaidia katika utendaji wao wa kazi.
Kikao kazi hicho kiliaanza rasmi Agosti 13 na kufunguliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki na yamefungwa rasmi Agosti 16 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.