Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe John V.K Mongella, ametembela na kukagua mradi wa Ujenzi wa shule mpya ya Msingi ya mikondo miwili, Nashooli Halmashauri ya Meru, ikiwa ni ziara yake ya kawadia ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mhe. Mongella licha ya kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, ametoa wiki moja kwa uongozi wa wilaya hiyo kupitia Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Meru, kukamilisha uwepo wa samani zote zinazohitajika na Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini wilaya (RUWASA), kuunganisha maji kwenye vyoo vyote shuleni hapo, kwa kuwa mifumo ya maji ipo tayari.
Aidha, ametumia muda huo, kuwakumbusha watalamu kuwa, Serikali imewapa dhamana kubwa ya kuwatumikia wananchi, ikiwa ni pamoja na kusimamia mali zote za Serikali katika maeneo waliyopangiwa kufanya kazi, hivyo ni vema kila mmoja akathamini na kutambua wajibu wake na kujituma bila kusubiri kusukumwa na viongozi wa ngazi za juu yake.
Amesema kuwa kila mtaalam, ameajiriwa kwa fani aliyosomea na kupewa nafasi kwenye eneo lake, hivyo kilq mmoja akiwajibika kwa nafasi yake, kulingana na fani yake kwa shirikiana na wenzake, kazi ya Serikali itakuwa rahisi na wananchi watapata huduma stahiki kama ilivyokusudiwa na si kusubiri kusukumwa na viongozi walio juu.
"Ili maendeleo ya Taifa hili yapatikane kila mtumishi anatakiwa kuwajibika kwa nafasi yake na kwa ngazi aliyopo, haiwezekani mtalamu kusubiri maelekezo kukukumbushwa na viongozi wa juu, tambueni na kuithamini dhamana kubwa mliyopewa na serikali iko siku mtailipia, wajibikeni shirikianeni pamojq na kushirikisha wananchi wa maeneo husika" Amesisitiza Mhe. Mongella
Awali, mradi huo umetekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 348.5, fedha kutoka serikali kuu kupitia mradi wa Kuboresha Upatikanaji wa Fursa sawa katika Ujifunzaji Bora kwa Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara (BOOST), uliojumuisha ujenzi wa Jengo la Utawala, vyumba vya madarasa, Madarasa ya awali ya mfano na matundu ya vyoo.
Ikumbukwe kuwa, miradi hiyo ya ujenzi wa miundombinu shule za msingi ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, Sura ya tatu Ibara ya 79 kifungu (q)Kukarabati miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na kifungu (C)Kuboresha uratibu na usimamiaji wa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.