Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, ametembelea mradi wa Kitovu cha Teknolojia za Kihandisi (KITEKI) Kijiji cha Gongali wilaya ya Karatu, mradi uliogharimu shilingi milioni 450.9 huku wananchi wa kijiji hicho, wakitoa eneo lenye ukubwa wa Ekari 3.
Mhe. Mongella licha ya kupongeza utekelezaji wa mradi huo, amewataka KITEKI, kutoa mafunzo kwa wakulima ya namna bora ya matumizi ya mashine hizo, huku akiwasisitiza kuuza na kukodisha mashine hizo kwa bei ambayo ni nafuu ili wakulima wote waweze kumudu kutumia zana hizo.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita, imejipanga kwawawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi ili kukabiliana na uhaba wa ajira pamoja na kuhakikisha huduma muhimu za jamii zinakuwa karibu na wananchi kulingana na mahitaji na vipaumbele.
"Tumeni kituo hiki kama sehemu ya kujifunza na kujipatia zana za kilimo na mifugo kwa bei nafuu, Serikali ya mama Samia, inataka kila mwananchi ajikite katika kufanya kazi za uzalishaji ili kukuza uchumi wa Taifa, Kupitia kituo hiki, muungeni mkono mama Samia kwa kufanya kazi kwa bidii" Amesisitiza Mhe. Mongella
Serikali imeanzisha mradi huo kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wakulima na wafugaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma za teknolojia za kihandisi hususani zana za kilimo, ufugaji, uvuvi ili kuongeza matumizi ya zana hizo na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Uwepo wa Teknolojia hizo karibu na wakulima, kutachangia ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na malighafi muhimu kwa ajili ya viwanda vidogo, ili kuboresha kipato na ustawi wa jamii pamoja na kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake nchini.
Hata hivyo, kituo hicho kitatoa huduma za uuzaji na ukodishaji wa mashine, kutoa mafunzo juu ya matumizi sahihi ya mashine kwa ajili ya kutatua changamoto katika sekta ya kilimo na mifugo pamoja na kuwa chanzo cha taarifa muhimu kwa wabunifu na kuwa chanzo cha upatikanaji wa mashine muhimu zinazotengenzwa nchini.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.