Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella, amekagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Soitsumb - Losirwa na Mailowa - Njoroi, zinazojengwa kwa fedha za ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwenye Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo wa Mfumo wa Ikologia wa Serengeti.
Mhe. Mongella amemtaka mkandarasi wa mradi huo, kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora kwa kuwa barabara hizo ni muhimu kwa wakazi wa Ngorongoro, mradi ambao unakwenda kuondoa kero ya usafiri kwa wananchi.
"Licha ya kuwa mmeongezewa muda wa utekelezaji wa mradi, hakikisheni mnakamilisha mradi huo kwa wakati, ili kuondoa kero zinazowakabili wananchi na zaidi kutimiza adhma ya Serikali ya kuhakikisha barabara zinapitika kipindi chote cha mwaka"Amesisitiza Mhe. Mongella
Akiwasilisha taarifa ya mradi, msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Richard Mwakasitu amesema kuwa, ujenzi huo wa barabra, unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9, ukijumuisha ujenzi wa barabara za Soitsumb - Losirwa yenye urefu wa Km 12.6 na barabara ya Mailowa - Njoroi yenye urefu wa Km 11, kwa kiwango cha moramu, mradi ambao unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba 2023.
Ameongeza kuwa lengo la kuboresha na kurahisisha hali ya usafiri wa wananchi na mali na kufika kwenye huduma zote za kijamii.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.