Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella amewataka watalamu wanaotoa huduma za afya kutoa huduma bora na stahiki kwa wagonjwa ili kuhakikisha wanapona na zaidi kufikia lengo la serikali la kupunguza idadi ya vifo visivyo vya lazima hususani kwa kina wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano.
Ametoa rai hiyo wakati akikagua dawa na vifaa tiba, vilivyoletwa na serikali mara baada ya kukamilika asilimia kubwa ya majengo kwenye Hospitali mpya ya wilaya ya Longido.
Mhe. Mongella amewataka Watoa huduma za Afya kufanya kazi kwa weledi kwa ya kuwahudumia wagonjwa kwa kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu pamoja wa ununuzi wa vifaa tiba.
Wahudumu wa afya mnapaswa kuzingatia nia ya serikali ya kuwekeza kwenye miundombinu hii ya afya ya kuhakikisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi, hivyo ni jukumu lenu kutimiza wajibu wenu ili kufikia lengo la serikali kwa kuwa mmepewa dhamana hiyo muhimu ya maisha ya watu.
"Mhe Rais anahangaika kutafuta fedha, fedha ambazo zimetolewa kujenga hospitali hii pamoja na dawa na vifaa tiba, hakikisheni kila mtumishi anatimiza wajibu wake ili wananchi wavutike kutumia huduma kwenye hospitali zetu za serikali, haiwezekani mwananchi ateseke wakati serikali yake imeshaandaa miundombinu bora ya kumpa huduma bora" Amesisitiza Mhe. Mongella
Ameongeza kuwa endapo mtatoa huduma bora mtawapunguzia wananchi gharama za kwenda hospitali ya Mount Meru na pia itapunguza msongamano wa wagonjwa waliokuwa wanafuata huduma Mount Meru na kuongeza kuwa serikali inataka kila mwananchi apate huduma zote ndani ya eneo analoishi jambo ambalo licha ya kupunguza gharama litaongeza utunzaji wa muda kwa wananchi wa kutafuta huduma za afya mbali.
Mradi huo umetekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.4, ambapo shilingi Bilioni 3 ni fedha kutoka Serikali Kuu hukunshilingi milioni 340 ni kupitia fedha za mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO 19.
Aidha hospitali hiyo inategemea kuhudumia zaidi ya wagonjwa 175,915 wa wilaya ya Longido na wengine kutoka Nchi jirani ya Kenya, kukiwa na lengo la kutoa huduma zote za afya pamoja na kupungumza gharama kwa wagonjwa kusafiri mpaka Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha, sambamba na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo ya Rufaa.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa hospitali za wilaya ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM wa kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na Hopitali kwa lengonla kusongeza huduma muhimu karibu na wananchi ikiwa na mapngo maalum wa kupambana na kuzuia vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
#arushafursalukuki
#kaziinaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.