Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella amemuelezea Marehemu Zelothe Stephene Zelothe aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi (mstaafu) wa Jeshi la polisi nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha, kuwa alikuwa ni Kiongozi aliyenyooka na mwenye msimamo kwa mambo ya msingi, muadilifu, mzalendo na mwenye kupenda watu na mwenye bidii katika kazi.
Mhe Mongella ameeleza hayo mara baada ya sala fupi iliyofanyika nje ya jengo la kuhifadhia maiti, Hosptali ya Rufaa ya mkoa wa Arusha, muda mfupi baada ya kuwasili mkoani Arusha na kuhifadhi mwili huo hospitalini hapo.
Ameanza kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa fursa aliyoitoa kwa maisha ya Mzee Zelothe hapa duniani, na kukiri kwamba kila mwanandamu anayosafari yake na mwisho huwa ni kifo na kusema kuwa marehemu Zelothe alikuwa ni Kiongozi hodari mwenye hekima nyingi na kauli thabiti, aliyenyooka na asiyekurupuka katika kufanya maamuzi.
Amethibitisha kuwa, katika kipindi chote ambacho mzee Zelothe amefanya kazi, akilitumikia Jeshi la Polisi kwa nafasi mbalimbali, akiwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkuu wa mkoa Rukwa na baadaye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa mkoa wa Arusha (NEC), amekuwa ni kiongozi mwenye nidhamu, mwadilifu, mwenye hekima, zaidi mwenye kupenda watu na kufanya kazi kwa bidii.
"Nachelea kusema Marehemu alikuwa ni mtu 'smart', amenyooka, asiye penda konakona, alipenda kufanya kazi kwa kushirikiana na wengine, aliwaunganisha watu na kuwa kitu kimoja, aliamini kwenye falsafa ya ushirikishwaji, alikuwa ni kiongozi na mwalimu wa kila mtu, sisi wengine tumejifunza mengi kutoka kwake" Amesema
Aidha amekiri kuwa ingawa pengo la mzee Zelothe halitazibika lakini ameahidi kuyaenzi maisha yake, na kuendeleza yale yote mema aliyoyafanya akiwa mtumishi wa Umma, kama baba, kama kiongozi na zaidi kama mwanachama muadilifu wa Chama Cha Mapinduzi.
Awali, Mrehemu Zelothe alifariki tarehe 26.10.2023 Jijini Dare es salaam akiwa napatiwa matibabu na mwili wake kuwasili Arusha 28.10.2023 huku mazishi yakitarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu 30.10.2023 nyumbani kwake kitongoji cha Olosiva kata ya Oloirieni wilaya ya Arumeru.
Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, Jina lake Lihimidiwe
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.