Na Elinipa Lupemne
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, ametoa salamu za pole kwa niaba ya Serikali, kwa familia, waombolezaji, ndugu, jamaa na marafiki, wakati wa ibaada maalum ya mazishi ya marehemu Nic Davie (Nisher), ambaye ni mtoto wa Nabii Mtume Geor Davie wa Kanisa la Ngurumo ya Upako, eneo la Kisongo mkoani Arusha.
Mhe. Mongella ametoa salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa pole kwa familia na wote walioguswa na msiba huo wa kijana wa kitanzania ambaye alikuwa akilitumikia Taifa katika fani ya Sanaa.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, ameniagiza kutoa pole kwa familia yako Mtume Geor Davie, Mhe. Rais amesema atakuja kukusalimu pindi atakapokuja Arusha". Amesema Mhe. Mongella
Hata hivyo amesema kwamba, serikali inathamini kazi inayofanywa na watumishi wa Mungu, ikiwemo huduma kubwa na maarufu ya Ngurumo ya Upako katika mkoa wa Arusha, huduma ambayo inawajenga wananchi kiroho na kusababisha mkoa kuwa na amani na utulivu.
Amebainisha kuwa, maendeleo ya mkoa wa Arusha na Serikali ya awamu ya sita, yanatokana na amani na utulivu wa wananchi wake, inayotokana hudma za kiroho, inayosababisha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji mali na na kukuza kipato.
Hata hivyo, amewataka wanaArusha kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano baina yao na kufanyakazi kwa bidii ili kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita.
Awali, Marehemu Nic Davie ( Nisher), alikuwa ni Mtayarishaji wa video mbalimbali za wanamuziki na filamu,muimbaji na mtunzi wa nyimbo, na amezikwa nyumbani kwao eneo la Kisongo, tarehe 16 Desemba, 2023.
Bwana Alitoa, Bwana Ametwa, Jina Lake Lihimidiwe
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.